Matokeo ya awali ya uchaguzi Uganda 2026, yalitolewa muda mfupi kabla ya saa tano usiku yanaonyesha Rais Yoweri Museveni wa NRM aliyemadarakani anaongoza kwa asilimia zaidi ya 60 ya kura zilizopigwa.
Jaji Simon Byabakama, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Uganda alisema matokeo hayo yamezingatia vituo 133 vya kupiga kura yaliowakilisha asilimia 0.26 ya jumla ya kura zilizopigwa.
Byabakama alithibitisha kuwa taarifa zingine juu ya uchaguzi zitatolewa Ijumaa, saa tatu asubuhi wakati matokeo zaidi yanaendelea kuwasilishwa katika kituo kikuu cha kuhesabu kura kilichoko eneo la Wakiso.
Awali, Jaji Byabakama alisema kuwa siku ya uchaguzi ilikwenda vizuri ingawa uchaguzi huo ulikumbwa na changamoto za hitilafu ya kimitambo ikiwa ni pamoja na mashine za kupiga kura zilizoshindwa kufanyakazi na kulazimisha shughuli ya upigaji kura kuendelea kwa njia ya kawaida.
Mgombea wa upinzani Robert Kyagulanyi amedai uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu.
“Matukio ya masanduku kujazwa kura yameripotiwa kila mahali,” alidai mgombea wa urais wa chama cha upinzani cha NUP Ssentamu Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa kijamii, bila kutoa uthibitisho madai hayo.
Mamlaka inayosimamia uchaguzi huo haijatoa kauli yoyote kuhusu madai ya udanganyifu katika uchaguzi, wala madai ya Wine kwamba mawakala “wengi” wa wapiga kura na wasimamizi wa chama chake cha NUP “walitekwa nyara, na wengine kufukuzwa katika vituo vya kupigia kura”.
Matokeo rasmi ya uchaguzi huu huo yanatarajiwa kutolewa ndani ya saa 48 baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika.