KINARA wa mabao wa Geita Gold, Maulid Shaaban amesema lengo alilonalo msimu huu ni kufunga mabao mengi katika mechi za timu hiyo ili mwisho wa msimu awe mfungaji bora katika Ligi ya Championship.
Shaaban hadi sasa amefunga mabao saba na asisti tano katika mechi 14 za ligi hiyo na anakamata nafasi ya tatu kwenye orodha ya wafungaji akiwa nyuma ya kinara, Adam Uledi wa Transit Camp mwenye mabao 10, Abdulrahman Mussa kutoka Gunners na Boniface Brown wa Mbeya Kwanza, wenye mabao nane kila mmoja.
Straika huyo analingana idadi ya mabao na Obrey Chirwa wa Kagera Sugar na Raymond Lulendi wa Songea United, walio na mabao saba kila mmoja.
Hivyo, mshambuliaji huyo wa zamani wa Coastal Union, Dodoma Jiji na Mbeya City ana kibarua cha kupindua meza na kutimiza malengo hayo katika mechi 16 zilizobaki za Ligi ya Championship.
Shaaban aliwahi pia kuwa kinara wa mabao katika ligi hiyo msimu wa mwaka 2023/2024 akifunga mabao 17 katika mechi 30 akiwa na Mbeya City, akifungana na William Edgar (Ken Gold) na Oscar Mwajanga (Mbeya Kwanza).
Akizungumza na Mwanaspoti, mchezaji huyo amesema amekuja Geita Gold msimu huu kuipandisha daraja kwa kushirikiana na wachezaji wenzake waliopo, hivyo atatumia uzoefu wake wa kucheza timu za Ligi Kuu kuisaidia timu hiyo kutimiza malengo yake.
“Tunashukuru Mungu msimu unakwenda vizuri na tumeshafika nusu ya malengo yetu, tumejiwekea malengo kuwa timu irudi Ligi Kuu na ndiyo itakuwa furaha yetu,” amesema Shaban na kuongeza;
“Kwa malengo yangu binafsi niliojiwekea ni kumaliza msimu niwe mfungaji bora wa ligi, hivyo nahitaji kufunga mabao mengi, hii itanisaidia pia kukua kwenye safari yangu ya soka na kutimiza ndoto ya kucheza nje ya nchi.”
Shaaban alisisitiza, msimu huu Geita imejipanga vyema kutorudia makosa ya msimu uliopita ambao iliishia kwenye mechi za mtoano kusaka nafasi ya kwenda Ligi Kuu.
“Tumejianda kwa kila idara kuakikisha hatuwezi kufanya makosa kama msimu ulioisha tutapambana mpaka tone la mwisho kuhakikisha tunairejesha timu Ligi Kuu,” amesema mshambuliaji huyo.