KOCHA wa Simba, Steve Barker  amewapongeza wachezaji wa timu yake kwa kuonyesha juhudi, nidhamu na ari ya kupambana baada ya ushindi wa mabao 3-0  dhidi ya Mtibwa Sugar ambao umeifanya  kuendelea kubaki kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Licha ya matokeo kuonekana ya kuridhisha kwenye karatasi, Barker amesema hakuridhishwa na namna timu yake ilivyoanza mchezo, akibainisha kuwa walikosa umakini wa kimwili na kiakili katika baadhi ya dakika za kipindi cha kwanza.

“Kwa kweli sidhani kama tulianza mchezo vizuri sana. Ingawa tulipata bao mapema, bado tulikosa ubora wa haraka na umakini wa kutosha kimwili na kiakili katika sehemu ya kipindi cha kwanza,” amesema Barker.

Kocha huyo amesema alilazimika kutumia maneno makali zaidi kwenye mapumziko ya kipindi cha kwanza ili kuamsha morali na kuongeza kiwango cha wachezaji wake kwa ajili ya kipindi cha pili.

“Tulizungumza na wachezaji na kuwaambia tunahitaji kuwa bora zaidi katika kila eneo la mchezo. Jibu lao la kipindi cha pili lilikuwa zuri sana na tuliweza kudhibiti mchezo vizuri zaidi,” amesema.

Barker pia hakuacha kuizungumzia hali ya uwanja, akisema haikuwa rahisi kwa Simba kucheza soka lao la pasi na kumiliki mpira kama wanavyopenda.

“Uwanja ulikuwa sawa na kusawazisha mambo. Haikuwa rahisi kucheza mchezo wetu wa kawaida wa kumiliki mpira na kupanga mashambulizi, lakini wachezaji walionyesha moyo wa kupambana na nidhamu hadi mwisho,” amesema.

Ushindi huo umeifanya Simba kusalia nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi iliwa na pointi 67, huku Yanga ikiendelea kuongoza kufuatia kuichapa Azam Kwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *