
Akizungumza katika Ukumbi wa Methodist Central Hall mahali palipofanyika Baraza Kuu la kwanza la Umoja wa Mataifa tarehe 10 Januari 1946 Bwana Guterres amewataka wajumbe wa tukio hilo kuwa “jasiri wa kutosha kubadilika. Jasiri wa kutosha kupata ujasiri wa wale waliokuja katika ukumbi huu miaka 80 iliyopita ili kuunda dunia bora.”
Kutoka kwenye hifadhi ya mabomu hadi mkutano wa kidiplomasia
Tukio la maadhimisho ya Jumamosi hii, lililoandaliwa na United Nations Association-UK, limekutanisha zaidi ya wajumbe 1,000 kutoka kote duniani. Miongoni mwa wazungumzaji walikuwemo Rais wa Baraza Kuu, Annalena Baerbock, Bingwa wa Umoja wa Mataifa kuhusu Masuala ya Anga Profesa Brian Cox, pamoja na Balozi wa Nia Njema wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, Maya Ghazal.
Tukio hilo pia limeadhimisha miaka 80 ya Baraza la Usalama la kwanza la Umoja wa Mataifa, lililofanyika tarehe 17 Januari 1946 katika Ukumbi wa Church House, karibu na hapo.
Katika hotuba yake kuu, Bw. Guterres ametafakari kuhusu umuhimu wa kihistoria wa mahali pa maadhimisho. Baraza Kuu la kwanza lilifanyika ndani ya kuta hizo hizo miezi minne baada ya kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, katika London iliyoharibiwa vibaya na mabomu ambako makumi ya maelfu ya watu walikuwa wameuawa kumbukumbu yenye nguvu ya kwa nini Umoja wa Mataifa uliundwa.
“Ili kufika kwenye ukumbi huu, wajumbe walilazimika kupita katika jiji lililojeruhiwa na vita. Ikulu ya Buckingham, Kanisa la Westminster Abbey, na Bunge la Uingereza zilishambuliwa na mabomu ya Luftwaffe. Na mabomu hayo yalipokuwa yakidondoka, raia waliokuwa na hofu walikusanyika hapa, kwenye chumba cha chini ya ardhi cha Methodist Central Hall moja ya makazi makubwa ya kujikinga na mashambulizi ya anga jijini London,” amesema Katibu Mkuu.
Wakati wa mashambulizi ya Blitz, hadi watu 2,000 walikuwa wakikusanyika katika ukumbi huo kwa ajili ya ulinzi, kabla ya mataifa ya dunia kukusanyika hapo mwaka 1946 kwa lengo la “kuokoa vizazi vijavyo dhidi ya janga la vita.”
“Kwa namna nyingi, ukumbi huu ni uwakilishi wa kimwili wa kile Umoja wa Mataifa ulivyo: mahali ambapo watu huweka imani yao kwa ajili ya amani, usalama, na maisha bora,” ametafakari Bwana Guterres.
Dunia ya mwaka 2026 si dunia ya mwaka 1946
Katika miaka 80 tangu Baraza Kuu la kwanza, Umoja wa Mataifa umekua kutoka wanachama 51 hadi 193. Bw. Guterres amesisitiza kuwa Baraza Kuu, chombo kikuu cha majadiliano, utungaji sera na uwakilishi cha Umoja wa Mataifa, ni “bunge la familia ya mataifa. Ni jukwaa la kila sauti kusikika, tanuru la maridhiano, na mwanga wa ushirikiano.”
Ingawa amekiri kuwa kazi ya Baraza Kuu “sio rahisi kila wakati au isiyo na changamoto,” aliielezea kama “kioo cha dunia yetu, migawanyiko yake na matumaini yake. Na ni jukwaa ambalo simulizi letu la pamoja huchezwa.”
Akirejea muongo uliopita, Bwana Guterres amesema kuwa “migogoro ya Gaza, Ukraine na Sudan imekuwa ya kikatili na ya kinyama kupita kiasi; akili mnemba (AI) imeenea kwa kasi kubwa; na janga la UVIKO-19 lilichochea moto wa utaifa likikwamisha maendeleo ya maendeleo na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.”
Amesisitiza kuwa mwaka 2025 ulikuwa “mgumu sana” kwa ushirikiano wa kimataifa na kwa maadili ya Umoja wa Mataifa.
“Misaada ilipunguzwa. Ukosefu wa usawa uliongezeka. Machafuko ya tabianchi yaliongezeka. Sheria za kimataifa zilikiukwa. Mashinikizo dhidi ya asasi za kiraia yaliongezeka. Waandishi wa habari waliuawa bila adhabu. Na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa walitishiwa mara kwa mara au kuuawa wakiwa kazini.”
Umoja wa Mataifa uliripoti mwaka 2025 kwamba matumizi ya kijeshi duniani yalifikia dola trilioni 2.7 — zaidi ya mara 200 ya bajeti ya sasa ya misaada ya Uingereza, au sawa na zaidi ya asilimia 70 ya uchumi wote wa nchi hiyo.
Mapato ya nishati ya mafuta (fossil fuels) pia ziliendelea kuongezeka huku sayari ikivunja rekodi za joto, amesisitiza Bwana Guterres.
“Na katika anga la mtandaoni, kanuni za kidijitali (algorithms) zilithawabisha uongo, kuchochea chuki, na kuwapa watawala wa kiimla zana zenye nguvu za udhibiti.”