
Hali hii imebainika kupitia uchambuzimpya wa Awamu Jumuishi ya Uhakika wa Chakula (IPC) uliozinduliwa leo tarehe 19 Januari 2026 na Wizara ya Kilimo ya Lebanon kwa ushirikiano na mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la Chakula na Kilimo (FAO) na la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).
Ingawa kuna dalili za utulivu wa muda ikilinganishwa na vipindi vilivyopita, uchambuzi huo unaonya kuwa uhakika wa kupata chakula katika taifa hilo la Mashariki ya Kati ni rahisi kuyumbishwa na mshtuko wa kiuchumi, kisiasa, na kiusalama.
Maeneo ya Baalbek, El Hermel, Akkar, na jamii za wakimbizi yameendelea kuathirika zaidi vibaya kutokana na madhara ya mizozo, ukosefu wa ajira, na upatikanaji mdogo wa huduma muhimu.
Waziri wa Kilimo nchini Lebanon, Dkt. Nizar Hani, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha sekta ya kilimo ili kujenga utulivu wa kudumu:
“Uhakika wa kupata chakula hauwezi kufikiwa kupitia misaada pekee, bali kupitia uwekezaji wa kimkakati katika uzalishaji wa ndani wa kilimo, ulinzi wa rasilimali asilia, na uwezeshaji wa jamii za vijijini kuchangia katika uchumi thabiti na endelevu wa kitaifa.”
Utabiri wa IPC kuanzia Aprili hadi Julai 2026 unaonesha kuwa idadi ya watu wenye uhaba wa chakula itaongezeka hadi kufikia 961,000 (sawa na asilimia 18).
Ongezeko hili linachochewa na upungufu wa misaada ya kibinadamu inayotarajiwa, gharama kubwa za maisha, na uharibifu wa miundombinu ya kilimo uliosababishwa na ukame mkali wa msimu wa 2024-2025.
Mwakilishi na Mkurugenzi wa WFP nchini Lebanon, Anne Valand, ameeleza wasiwasi wake kuhusu hatari inayowakabili wananchi:
“Nyuma ya takwimu hizi kuna familia ambazo zimebakiwa na mshtuko mmoja tu kabla ya kurudi tena kwenye hali mbaya ya uhaba wa chakula. Mahitaji ya watu bado ni makubwa, na misaada inayotabirika itakuwa muhimu sana ili kuwasaidia watu kupata mahitaji ya msingi ya chakula na kuzuia hali kuzorota zaidi.”
Kwa upande wake, Mwakilishi wa FAO nchini Lebanon, Nora Ourabah Haddad, amebainisha kuwa wakulima wadogo ni miongoni mwa watu walioathirika zaidi:
“Takriban nusu ya kaya za wakulima wameripoti kupungua kwa chanzo chao kikuu cha mapato kutokana na athari mbayá za mzozo na ukame wa muda mrefu. Kwa hiyo, FAO inatoa kipaumbele katika kurejesha maisha ya kilimo na kulinda mashamba, kwani uwekezaji endelevu katika kilimo ni muhimu ili kulinda mafanikio yaliyopatikana.”
Hata baada ya mwaka mmoja tangu kusitishwa kwa mapigano mnamo Novemba 2024, uchambuzi huu unasisitiza kuwa Lebanon bado inahitaji ufuatiliaji wa karibu na hatua za pamoja za kimataifa ili kulinda watu walio katika mazingira magumu zaidi na kuzuia janga kubwa la njaa mwaka 2026.