
Ingawa mwelekeo wa dunia kwa ujumla unaendelea kuelekea kufutwa kabisa kwa adhabu ya kifo, tathimini hiyo ya Umoja wa Mataifa inasema idadi ya kunyongwa imeongezeka kwa kasi hasa kwa makosa yasiyofikia kigezo cha “makosa makubwa zaidi kinachotambuliwa na sheria ya kimataifa”.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, amesema ofisi yake imebaini “ongezeko la kutisha la matumizi ya adhabu ya kifo mwaka 2025,” likihusisha kunyongwa kwa makosa ya dawa za kulevya, kunyongwa kwa watu waliotiwa hatiani kwa makosa waliyotenda wakiwa watoto, pamoja na ukosefu wa uwazi kuhusu utekelezaji wa hukumu hizo.
Amesema “Hili linaenda kinyume na sheria ya kimataifa na pia halisaidii kuzuia uhalifu.”
Ikitoa mfano imesema Iran imerekodi idadi kubwa zaidi ya kunyongwa duniani, ambapo takriban watu 1,500 waliuawa mwaka 2025. Karibu asilimia 47 walinyongwa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.
Türk amesema “kasi na ukubwa wa kunyongwa vinaashiria matumizi ya kimfumo ya adhabu ya kifo kama chombo cha vitisho vya dola, huku makundi ya makabila ya wachache na wahamiaji yakiathirika zaidi”.
Nchini Saudi Arabia, kwa mujibu wa tathimini angalau watu 356 walinyongwa mwaka 2025ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa nchini humo. Asilimia 78 ya hukumu hizo zilihusiana na makosa ya dawa za kulevya.
Türk ameongeza kuwa “takriban watu wawili kati ya waliouawa walihukumiwa kwa makosa waliyotenda wakiwa watoto, hali inayozua maswali mazito kuhusu haki za watoto.”
Hapa nchini Marekani, imeelezwa kuwa watu 47 walinyongwa mwaka 2025 ikiwa ni idadi kubwa zaidi katika kipindi cha miaka 16. Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi kuhusu matumizi yanayoongezeka ya gesi ya kuua kwa kukosa hewa, ukionya kuwa inaweza kufikia kiwango cha mateso au adhabu za kikatili.
OHCHR imesema kunyongwa hadharani kuliendelea nchini Afghanistan, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa hukumu kwa watu wanne katika viwanja vya michezo mwezi Aprili mwaka jana, jambo linalokiuka wazi sheria ya kimataifa.
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umetambua hatua chanya zilizochukuliwa na baadhi ya nchi, zikiwemo Zimbabwe iliyofuta adhabu ya kifo kwa makosa ya kawaida, pamoja na mageuzi ya kisheria nchini Malaysia, Pakistan, Vietnam, Kenya na Kyrgyzstan.
Türk amesema “Adhabu ya kifo si chombo bora cha kudhibiti uhalifu. Inaweza kusababisha kuuawa kwa watu wasio na hatia na mara nyingi hutekelezwa kwa njia ya kiholela na ya kibaguzi.”
Kamishna Mkuu ametoa wito kwa nchi zote zinazotumia adhabu ya kifo kuweka mfumo wa kusitishwa mara moja kwa utekelezaji wa hukumu hizo, kubadili hukumu zilizopo, na kuelekea kufutwa kabisa kwa adhabu ya kifo.