Akihutubia Baraza hilo kwa njia ya video kutoka The Hague, Uholanzi, Naibu Mwendesha Mashtaka wa ICC, Nazhat Shameem Khan, amesema El Fasher imekuwa kitovu kipya cha mauaji ya kikatili ya halaiki huko Darfur, hali inayodhihirisha muendelezo wa mifumo ya vurugu ambayo imeikumba kanda hiyo kwa miaka mingi.

Mgogoro unashika kasi kila uchao

Amesisitiza kuwa mgogoro huo hauendelei tu, bali unazidi kushika kasi, ukichochewa na kile alichokitaja kama “hali ya kutokuwajibishwa kabisa.”

Kwa mujibu wa ICC, kuanguka kwa El Fasher mikononi mwa  RSF kuliambatana na kampeni iliyopangwa na ya makusudi ya mateso makubwa, hasa ikilenga jamii zisizo za kiarabu.

Bi. Khan ambaye alieleza usuli wa kuhutubia kwa video badala ya kufika ukumbini ni kunyimwa kibali cha kuingia Marekani, ametaja ubakaji, kukamatwa kiholela, mauaji ya kinyama, na kuanzishwa kwa makaburi ya halaiki, vyote vimefanyika kwa kiwango kikubwa.

Baadhi ya uhalifu huo, amesema, ulirekodiwa kwa video na kusherehekewa waziwazi na walioutekeleza, jambo linaloonesha ukosefu mkubwa wa hofu au uwajibikaji.

Maoni ya kina ya mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili hali nchini Sudan na Sudan Kusini, na wajumbe wameketi karibu na meza kubwa ya mviringo na video ya kulisha iliyoonyeshwa kwenye skrini.

Picha ya UM/Manuel Elías

Taswira ya ukumbi wa Baraza la Usalama jla Umoja wa Mataifa lilipokutana Jumatatu Januari 19, 2026 kujadili hali nchini Sudan na Sudan Kusini.

Ushahidi wathibitisha uhalifu wa kivita na dhidi ya binadamu

Kulingana na ushahidi uliokusanywa katika kipindi cha hivi karibuni cha utoaji taarifa yaani kati ya Agosti hadi Desemba mwaka 2025, ukiwemo video, sauti na picha za setilaiti, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa ICC imehitimisha kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu ulifanyika El Fasher, hasa mwishoni mwa Oktoba, kufuatia kuzingirwa kwa mji huo na RSF.

Taarifa zilizochambuliwa zinaonesha mifumo ya uhalifu inayofanana na ile iliyoshuhudiwa awali katika maeneo mengine ya Darfur: kuwazuia raia kusaka usalama, kuwatesa, na kuwaua watu kutoka makabila yasiyo ya kiarabu, pamoja na kudhalilisha miili baada ya mauaji.

Picha za setilaiti zilizochunguzwa na wachunguzi zinaashiria matukio ya mauaji ya halaiki na juhudi za kuficha uhalifu huo kupitia kuanzishwa kwa makaburi ya pamoja.

Matokeo haya yamehakikiwa kupitia mawasiliano na jamii zilizoathirika, mashahidi wanaowezekana, na taarifa zilizowasilishwa na mashirika ya kiraia.

Taswira inayojitokeza, Khan amewaeleza wajumbe wa Baraza, ni ya “uhalifu uliopangwa, ulioenea na wa kiwango kikubwa,” ambapo mauaji ya kikatili yanatumika kama nyenzo ya kudhibiti maeneo.

Kukamatwa kwa Al Bashir

Bi. Khan amezungumzia pia hati za kukamatwa kwa watuhumiwa wa uhalifu wa kivita akisema, “ningependa pia kuwa wazi kuhusu jambo moja muhimu: serikali ya Sudan lazima ifanye kazi na sisi kwa kwa umakini, kuhakikisha kukamatwa kwa watu walioko chini ya amri za kukamatwa za ICC waliopo Sudan kwa sasa: Omar Hassan Ahmad Al Bashir, Ahmad Harun na Abdel Raheem Muhammad Hussein.”

Amesema anaweka mkazo tena kuwa Harun  lazima apewe kipaumbele. “Hatua lazima zichukuliwe sasa kumfikisha mahakamani au kuhakikisha anajikabidhi kwa hiari.”

Bila uwajibikaji, hali itazidi kuwa tete Darfur

Khan ameonya kuwa bila kuwepo kwa uwajibikaji na kukomeshwa kwa hali ya kutoadhibiwa inayotawala, mzunguko wa vurugu utaendelea kusambaa “kutoka mji mmoja hadi mwingine” kote Darfur.

Amewataka wajumbe wa Baraza la Usalama kuvuka hatua ya kauli za wasiwasi na kuchukua hatua za dhati za kuwalinda raia na kuunga mkono juhudi za haki.

Ujumbe wa ICC ni wazi: kinachotokea El Fasher si tukio la pekee, bali ni onyo la kuongezeka kwa mauaji ya kikatili Darfur—mauaji ambayo yataendelea isipokuwa jumuiya ya kimataifa ichukue hatua za haraka na madhubuti kuhakikisha uwajibikaji na kuwalinda raia walio hatarini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *