
Makamanda na wanajeshi wa majini ya China na Afrika Kusini wametembelea meli za kivita za kikosi cha majini cha Iran kilichotia nanga katika bandari ya Cape Town, pembeni mwa mazoezi makubwa ya kimataifa ya majini yanayoandaliwa na Afrika Kusini.
Ziara hizo zilifanyika wakati majeshi ya majini kutoka Iran, China, Afrika Kusini na nchi kadhaa za Brics yakishiriki mazoezi ya pamoja ya majini yajulikanayo kama Azma ya Amani (Will for Peace0 2026.
Wanamaji kutoka kikosi cha majini cha China, ambacho kilitia nanga Cape Town kwa ajili ya kushiriki mazoezi hayo, walipanda meli za Iran kukutana na wenzao wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ziara hiyo ilijumuisha meli ya kivita ya Makran, manowari ya Shahid Naghdi ya Jeshi la Wanamaji la Iran, pamoja na meli ya kivita ya Shahid Mahdavi ya Jeshi la Wanamaji la Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
Wanamaji wa Jeshi la Wanamaji la Afrika Kusini pia walipanda meli hizo hizo za kivita za Iran, na kukutana na makamanda wa Kiirani ambapo walifanya mazungumzo yaliyolenga ushirikiano na kubadilishana uzoefu.
Lengo la ziara hiyo lilielezwa kuwa ni kujenga mawasiliano ya ana kwa ana na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma, hatua inayolenga kuimarisha uhusiano kati ya majeshi ya majini ya nchi hizo.
Admeri Mkuu Monde Lobese, kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Afrika Kusini, alitembelea binafsi meli za kivita za Iran zinazoshiriki katika mazoezi hayo, akikagua sehemu mbalimbali za meli za Makran, Shahid Naghdi na Shahid Mahdavi.
Wakati wa ziara hiyo, Kamanda Lobese alikumbuka safari yake ya awali nchini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akisema ilimpa fursa ya kufahamu uwezo mkubwa na uwezo mpana wa kiutendaji wa Jeshi la Wanamaji la Iran.
Aliongeza kuwa uwepo wa kikosi cha majini cha Jamhuri ya Kiislamu mjini Cape Town ni jambo muhimu na lenye thamani kwa Afrika Kusini, akiitaja Iran kama taifa la ndugu na rafiki.
Ziara hizo zilikuwa sehemu ya mazoezi mapana ya pamoja ya majini ya nchi za kundi la BRICS Plus yanayofanyika katika maji ya pwani ya Afrika Kusini.
Mazoezi hayo yalijumuisha majeshi ya majini kutoka Iran, China, Russia, Afrika Kusini, Ethiopia, Indonesia, Brazil, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Katika ushiriki wake, Iran ilituma rasilimali kadhaa za kijeshi za majini, ikiwemo meli tatu zilizotajwa.