
Mahakama ya rufaa nchini Tunisia siku ya Jumatano imethibitisha kifungo cha miaka 22 jela dhidi ya Rached Ghannouchi, kiongozi wa Harakati ya Ennahda na aliyekuwa Spika wa Bunge, katika kesi maarufu ya Instalingo.
Uamuzi huo umeidhinisha hukumu za awali dhidi ya wanasiasa, wanahabari, wanablogu na wafanyabiashara 40, huku ukibadilisha hukumu ya mshtakiwa mmoja wa kike na kuamuru aachiwe huru, kwa mujibu wa vyanzo vya mahakama vilivyonukuliwa na vyombo vya habari vya serikali.
Mnamo Februari 5, mahakama ya chini ilitoa vifungo vinavyotofautiana kati ya miaka 5 hadi 54 kwa washtakiwa 41, akiwemo Ghannouchi, mwenye umri wa miaka 84, ambaye amekuwa kizuizini tangu Aprili 17, 2023. Tangu wakati huo amehukumiwa mara kadhaa katika kesi tofauti.
Washtakiwa wote wamekanusha mashtaka yanayowakabili, ambayo ni pamoja na kushirikiana dhidi ya usalama wa taifa, kujaribu kubadili mfumo wa dola, kuchochea Watusinia kukabiliana kwa silaha, kusababisha vurugu na uporaji, na kutenda vitendo vya uhasama dhidi ya rais.
Katika sheria za Tunisia, shtaka la “kitendo cha uhasama dhidi ya rais” linahusisha mwenendo unaoonekana kuwa shambulio kubwa dhidi ya mtu au mamlaka ya mkuu wa nchi, ikijumuisha vitisho, mashambulizi ya kimwili au hatua zinazodhoofisha mamlaka ya dola.
Mamlaka ya Tunisia yamesisitiza kuwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya jinai bila kuingiliwa kisiasa. Hata hivyo, wapinzani wanasema kesi hii ni sehemu ya kampeni pana ya kuwalenga wakosoaji wa hatua za kipekee zilizochukuliwa na Rais Kais Saied.
Mnamo Julai 25, 2021, Saied alitangaza hatua za kipekee zilizojumuisha kuvunja bunge, kutawala kwa dikrii, kuandaa katiba mpya kupitia kura ya maoni, na kufanya uchaguzi wa mapema wa wabunge.
Upinzani umeeleza hatua hizi kama mapinduzi dhidi ya katiba na mwelekeo wa utawala wa mtu mmoja, ilhali wafuasi wake wanadai kuwa zilirekebisha mwelekeo wa mapinduzi ya 2011 yaliyomuondoa madarakani Zine El Abidine Ben Ali.
Saied amesisitiza mara kwa mara kuwa hatua zake ziko ndani ya mipaka ya katiba na zinalenga kulinda taifa dhidi ya hatari iliyo karibu, huku akidai kuwa haki na uhuru havijapunguzwa.