Waziri wa Ulinzi wa Iran, Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh, amemuonya yeyote anayewatishia watu wa Iran kwa shambulio la kijeshi, akisema kwamba Tehran ina “mastaajabu ya kukabiliana na vitisho hivyo, na washambuliaji watapata maumivu na mateso makubwa kwa mastaajabu hayo.”

Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh ametangaza kwamba iwapo pande zinazotishia “zitafanya upumbavu wowote na kushambulia maslahi ya nchi yetu, tutalenga maslahi yao yote popote duniani,” akiongeza kwamba: “Nchi yoyote itakayowezesha shambulio hilo au kumpa mshambuliaji kambi zake za kijeshi, itakuwa shabaha halali.”

Amewataja wanasiasa wanaotoa vitisho dhidi ya Iran kuwa “wana maono finyu,” akisema kwamba wanapaswa “kuona adhama ya watu wa Iran, na kutambua kwamba nguvu zetu ziko hasa katika watu hawa.”

Matamshi haya ya Waziri wa Ulinzi wa Iran yanafuata kauli ya Donald Trump siku ya Jumapili ambaye alidai kwamba anafikiria “chaguo kali” dhidi ya Iran, ikiwa ni pamoja na hatua zinazowezekana za kijeshi kuhusu kile alichokiita “ukandamizaji” wa Jamhuri ya Kiislamu wa waandamanaji.

Kabla ya hapo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi alikuwa  ameionya Marekani kwamba Tehran “iko tayari kwa machaguo yote” baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Katika mahojiano yake na televisheni ya Al Jazeera jana Jumatatu, Araqchi alisema njia za mawasiliano na Marekani ziko wazi, lakini akisisitiza kwamba Tehran iko tayari kwa vita ikiwa Washington inataka “kujaribu”.  

Sayyid Abbas Araqchi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa Iran sasa ina “maandalizi makubwa na mapana ya kijeshi” ikilinganishwa na wakati wa Vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na Marekani na Israeli mwezi Juni mwaka jana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *