Rais wa zamani wa mpito wa Burkina Faso, anayedaiwa kuwa mpangaji mkuu wa njama kadhaa za mapinduzi, amekamatwa na kufukuzwa nchini Togo.

Paul-Henri Sandaogo Damiba alimpindua Rais wa Burkina Faso, Roch Marc Christian Kaboré, katika mapinduzi ya 2022. Lakini miezi minane baadaye, Damiba mwenyewe alipinduliwa na kiongozi wa kijeshi, Ibrahim Traoré, ambaye bado yuko madarakani.

Ripoti zinasema Damiba alikamatwa huko Lomé wiki iliyopita na kushtakiwa kwa jaribio la kuyumbisha amani nchini Burkina Faso. Baadaye alipelekwa uwanja wa ndege, ingawa haijukani ameelekea wapi.

Tangu alipokwenda uhamishoni nchini Togo, Damiba ameshutumiwa kwa njama nyingi za mapinduzi na mauaji.

Ouagadougou inasema serikali imebatilisha jaribio la kumuua Traoré lililopangwa kufanyika tarehe 3 Januari.

Watu kadhaa wanaodaiwa kula njama ya mapinduzi wameonekana kwenye televisheni ya serikali, wakidai kutenda kwa amri ya Damiba.

Maafisa wa usalama wa Burkina Faso wanasema Damiba alikuwa amepanga mauaji kadhaa yaliyolenga raia na wanajeshi, yakianza na kiongozi wa sasa wa nchi hiyo, Ibrahim Traoré.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *