Maafisa wa usalama na taasisi za ujasusi za Iran zimewakamata zaidi ya watu 470 katika mikoa mitatu, waliotambuliwa kama watu muhimu na vinara wa wimbi la hivi karibuni la machafuko ya vurugu na harakati za kigaidi zinazohusiana na mitandao inayoungwa mkono na madola ya kigeni.

Ofisi ya Wizara ya Intelijensia ya mkoa ya Khorasan Razavi ilitangaza jana Jumatatu kwamba imewakamatwa magaidi 192 wenye silaha, waliotambuliwa kama mawakala wakuu waliohusika na ghasia za hivi karibuni katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, watuhumiwa hao walihusika katika mauaji ya maafisa kadhaa wa usalama na raia, kuchoma moto misikiti, vituo vya huduma za umma na mabasi, pamoja na mashambulizi dhidi ya vituo vya kijeshi na vya kutekeleza sheria.

Vifaa vilivyokamatwa kutoka kwa kundi hilo ni pamoja na fulana kadhaa za kuzuia risasi, bunduki za Kalashnikov, silaha za uwindaji, bunduki za Winchester, na silaha mbalimbali baridi kama vile majambia, mapanga, visu, pinde za msalaba na minyororo.

Ushahidi unaonyesha kwamba baadhi ya watu hao walikuwa na uhusiano na harakati za uadui na mashirika ya kigaidi, wakiwa na uhusiano na watu wa ng’ambo. Wengine walitambuliwa kama wanachama wa magenge ya wahalifu makatili, wakishiriki kikamilifu katika machafuko pamoja na washirika wao.

Wakati huo huo, katika mkoa wa magharibi wa Lorestan, IRGC imetangaza kukamatwa watu 134 kama viongozi wakuu na mawakala wenye ushawishi mkubwa wa mtandao wa kigaidi unaofadhiliwa na Marekani na Israel.

Taarifa ya IRGC imesema kwamba watu hao waliunda vikundi vya kigaidi wakati wa machafuko ya hivi karibuni, wakifanya vitendo “kama vya Daesh”.

Walijeruhi askari usalama kwa silaha za moto na baridi, na kuchoma na kuharibu mali za umma na za kibinafsi, ikiwa ni pamoja na misikiti, maduka, benki na magari ya watu binafsi na ya umma.

Katika mkoa wa kaskazini magharibi wa Zanjan, polisi waliripoti kuwakamata watu 150 waliotambuliwa kama viongozi wakuu na mawakala nyuma ya ghasia za hivi karibuni hapa nchini.

Wakati wa machafuko hayo, mamluki walioungwa mkono na madola ya kigeni walivamia miji, wakiwaua askari usalama na raia na kuharibu mali ya umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *