
Waislamu wa India wamefanya maandamano katika mji wa Ahmedabad, kupinga kuondolewa majina yao kwenye orodha ya wapiga kura kwa kisingizio kwamba wamefariki dunia, ingawa bado wako hai.
Vyanzo vya habari vya ndani vimeripoti kwamba majina ya mamia ya Waislamu yameondolewa kwenye orodha ya wapiga kura katika majimbo ya uchaguzi yenye Waislamu wengi ya Daryapur na Jamalpur huko Ahmedabad, baada ya kujaza fomu za usajili na majina yao kusajiliwa kwenye orodha ya awali ya wapiga kura.
Video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya India imeonyesha Waislamu wakishiriki katika kampeni ya maandamano, wakiwa na karatasi zenye majina ya wale wanaodaiwa kufariki dunia, ingawa bado wako hai.
Waislamu na wanachama wa chama cha mrengo wa kushoto cha Congress wamekituhumu Chama cha Bharatiya Janata cha mrengo wa kulia kuwa kinahusika kujaza fomu zenye majina ya wapiga kura Waislamu na kuwasilisha maombi ya kuwatangaza kuwa wamekufa, jambo lililosababisha majina yao kuondolewa kwenye orodha ya wapiga kura.
Katika muktadha huu, Kamati ya Uratibu ya Wachache nchini India imemwandikia afisa mkuu wa uchaguzi huko Gujarat, ikimtuhumu kwa majaribio ya kuwaondoa wapiga kura Waislamu kwenye orodha ya wapiga kura katika eneo bunge la Jamalpur huko Ahmedabad.
Kamati hiyo imeyataja matukio hayo kuwa ni “jitihada za makusudi za chama cha siasa zinazolenga kupunguza ushawishi wa wapiga kura Waislamu” nchini India.