Rais Vladimir Putin wa Russia amesema ikiwa Marekani itaipatia Ukraine makombora aina ya Tomahawk ili kufanyia mashambulio ya masafa marefu ndani ya Russia, hatua hiyo itapelekea kuvurugika husiano wa Moscow na Washington.

Putin ameyasema hayo katika klipu ya video iliyotolewa siku ya Jumapili akisisitiza. “hii itapelekea kuvurugika uhusiano wetu, au kwa uchache mwelekeo mzuri ambao umejitokeza katika uhusiano huu”. 

Mwezi uliopita, Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance alisema, Washington inazingatia ombi la Ukraine la kupatiwa makombora ya masafa marefu aina ya Tomahawk ambayo yanaweza kushambulia maeneo ya ardhi ya Russia, ikiwa ni pamoja na mji mkuu Moscow, ingawa haijajulikana kama Washington imeshachukua uamuzi wa mwisho juu ya ombi hilo au la.

Makombora ya Tomahawk yanafika umbali wa kilomita 2,500 (maili 1,550), ikiwa na maana kwamba endapo Ukraine itapatiwa makombora hayo na Marekani, ikulu ya rais, Kremlin na eneo lote la ardhi ya Russia lililoko upande wa Ulaya yatakuwa shabaha na mlengwa wa makombora hayo.

Siku ya Alkhamisi iliyopita, Rais wa Russia alisema, haiwezekani kutumia makombora ya Tomahawks bila ya ushiriki wa moja kwa moja wa wanajeshi wa Marekani, kwa hivyo usambazaji wowote wa makombora kama hayo kwa Ukraine kutachochea “hatua mpya ya kuongezeka kwa makabiliano”.

Putin ametoa indhari hiyo huku mapigano yakiendelea kushtadi katika uwanja wa vita, huku Russia ikizidi kusonga mbele kwa mashambulizi makubwa inayofanya dhidi ya Ukraine. ../

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *