Kipindi hiki kinahusu mpango mkuu wa AI wa Marekani, matumizi yake ya kijeshi, vyombo vya habari, uwekezaji, umuhimu wa kielimu na ushindani wa kimataifa.

Wasikilizaji wapendwa wa Redio Tehran katika makal yetu hii ya wiki tumedhamiria kuchunguza kadhia ambayo hivi sasa imekuwa moja ya mihimili muhimu sana duniani: Teknolojia ya akili mnemba (AI) na mchango wake katika vyombo vya habari, kisiasa, kiuchumi na katika usalama wa kimataifa. 

Tukio la karibuni katika uwanja huu ni hatua ya Marekani ya kuzindua mpango mkubwa wa akilii mnemba. Kidhahiri mpango huo ulibuniwa huku malengo yake yakiwa ni kuharakisha uvumbuzi wa kiteknolojia, kustawisha miundombinu ya kitaifa na kuimarisha nafasi ya Marekani katika kuongoza mchakato wa dunia wa ustawi wa akili mnemba.  

Hata hivyo vyombo vya habari vimeitaja hatua hii kuwa aina fulani ya kengele ya tahadhari kwa nchi nyingine duniani. Kwa mujibu wa chambuzi mbalimbali, nchi ambazo hazijawekeza na kutekeleza sera zinazohitajika katika uga wa akili mnemba zinakabiliwa na uwezekano wa kusalia nyuma katika mchakato wa kimataifa wa kukuza teknolojia hiyo na kushindwa kulinda nafasi yao ya ushindani sambamba na kuathiriwa na ukiritimba kuhusu suala hilo katika siku zijazo. 

Kwa mujibu wa tangazo rasmi la serikali ya Marekani, nchi hiyo imetenga dola bilioni 50 kwa ajili ya kustawisha miundo msingi muhimu ya akili bandia (AI). Kiwango hiki ni mara mbili ya bajeti ya kijeshi ya nchi kama China na kinaonyesha umuhimu wa kistratejia wa teknlojia hii kwa wanasiasa wa Marekani ili kudumisha ushawishi wao duniani. 

Mbali na uwekezaji mkubwa uliofanywa, hati yenye kurasa 28 kwa jina “Mpango wa Utekelezaji wa Akili Mnemba wa Marekani” imechapishwa. Hati hiyo inajumuisha hatua 90 za kisiasa ambazo zinafuatilia masuala makuu matatu: Kuongeza kasi ya uvumbuzi wa kiteknolojia, kuunda na kuimarisha miundombinu ya kitaifa ya AI na diplomasia na usalama wa kimataifa.

Katika uga wa kuzidisha kasi ya uvumbuzi wa kiteknolojia, matumizi ya akili bandia yameonekana kuwa na umuhimu mkubwa ndani ya serikali na katika jeshi la Marekani. kwa mfano, jeshi la Marekani linaendeleza mifumo miwili ya akili bandia kwa majina ya  Camo GPT na NiprGT.  Mifumo hii inafanya kazi nyingi: Kutabiri ukarabati wa vifaa, kugawa na kuchanganua mawasiliano ya nchi zisizofungamana na upande wowote ambazo Marekani inaziona kuwa adui, huku ikiboresha vifaa na kuchambua njia mbalimbali za oparesheni. 

Pia vyombo vya habari vimeripoti kuhusu kudhihiri aina mpya ya ndege zisizo na rubani katika mpango wa kijeshi wa Marekani kwa jina la droni mama. Sababu ya kupewa jina hilo ni kwamba ndege hizo zinaweza kubeba hadi droni ndogo mia moja na kuziongoza kwa mfumo wa akili mnemba. Teknolojia hii imebuniwa kwa namna ambayo ndege hizo zina uwezo wa kukusanya taarifa muhimu na kutekeleza misheni iliyoamuliwa mapema bila ya kuhitajia kuongozwa moja kwa moja na binadamu. 

Weledi wa mambo wanasisitiza kuwa matumizi ya aina hii ni mfano mmoja tu wa teknolojia ya akili mnemba, ambayo inadhihirisha uwezo wake katika mazingira changamano na magumu. Kuanzia kukusanya taarifa hadi kuchukua maamuzi, yote haya ni mifano ya nafasi kuu na muhimu ya akili bandia katika usalama wa baadaye na ulinzi wa nchi. 

Kwa mtazamo wa kisayansi, Chuo Kikuu cha Stanford kimesema katika ripoti kwamba akili bandia ni teknolojia ya msingi, sawa na umeme au mtandao, ambayo inaweza kuimarisha nyanja nyingine za sayansi na viwanda na kubadilisha jamii, uchumi na siasa. Umuhimu mkubwa wa teknolojia hii umezipelekea nchi mbalimbali kutekeleza sera kuu na kuwekeza pakubwa katika uwanja huo.

Katika ushindani wa kimataifa, Marekani ni mfano mkuu lakini China pia inastawisha kwa jadi miundombinu na teknolojia zinazofanana. Mchuano huu wakati mwingine hujulikana kama “Vita Baridi vya AI”, kwa sababu nchi zote mbili zinajua vyema kwamba kumiliki ujuzi wa AI kunaweza kuainisha nafasi yao ya kimkakati duniani.

Wakati huo huo, matamshi ya Trump pia yanaapsa kuzingatiwa. Alisema: “Serikali yangu itatumia zana zote ilizonazo ili kuhakikisha kwamba Marekani inajenga na kudumisha miundombinu mikubwa zaidi, yenye nguvu  na ya hali ya juu ya akili mnemba duniani.” 

Matamshi haya kwa hakika yanaonyesha azma ya kupiga hatua kiteknolojia,  lakini wakati huo huo ni indhari kuu.  Iwapo harakati hii itaendelea bila ya uwiano na ushirikiano wa kimataifa, itapelekea kuimarika misimamo ya upande mmoja ya Marekani katika uga wa teknolojia; hali ambayo si tu inawaweka pembeni washindani na washirika wa kimataifa, bali pia inabadili muundo wa siku zijazo wa akili mnemba kuwa zana ya kuimarisha udhibiti wa kisiasa na kiuchumi wa Marekani.

Hii ina maana kwamba ushindani si tu wa kisayansi au kiuchumi; bali ni mashindano ya kijiografia na kisiasa. Marekani inataka kuhakikisha kuwa imezitangulia nchi zote na washirika wake wana teknolojia wanazohitaji ili wasipitwe na China. Ni wazi kuwa kwa mtazamo huu, Washington inajaribu kufafanua kuwa akili  bandia si tu ni wenzo wa wa maendeleo, bali pia ni nguzo mpya ya nguvu zake  duniani; nguzo ambayo iwapo itaachwa kwa upande mmoja mikononi mwa Marekani, itakuwa chombo cha kulazimisha matakwa yake kwa nchi nyingine, na hivyo kuuweka katika hali ya kulegalega mlingano wa kimataifa.

Sera hizi zinaonyesha kwamba akili mnemba kabla ya kuwa teknolojia ya kielimu au kiviwanda, imekuwa kipengele cha kimkakati katika diplomasia na usalama wa kimataifa. Marekani inafanya hivi lengo likiwa ni kupiga hatua kiteknolojia na kuwazuia mahasimu wake wakuu kupiga hatua haraka khususan China. 

Suala hili pia limezingatiwa na vyombo vya habari ambavyo vinatoa uchambuzi wake kwamba udhibiti na uwekezaji katika akili bandia unaweza kuainisha uwezo wa nchi mbalimbali duniani. Kwa msingi huo, teknolojia hii sio tu ni chombo cha kielimu, bali pia ni chombo muhimu cha ushindani wa kijiografia na kiuchumi.

Katika sekta ya miundombinu, lengo la Marekani ni kuendeleza mitandao, vituo vya data, mifumo ya kompyuta ya wingu na kuasisi viwango vya kitaifa vya AI. Lengo ni kuhakikisha kuwa zana na miundombinu yote muhimu ya kuharakisha ubunifu inapatikana na hakuna mapungufu yoyote ya kiteknolojia.

Katika nyanja ya diplomasia na usalama, sera ya Marekani imejikita katika kuwapatia waitifaki wake teknolojia ya akili mnemba (AI) ili kuimarisha satwa na nafasi yake duniani na kuzuia China kupiga hatua katika nyanja hiyo. Kwa maneno mengine ni kuwa, akili bandia sasa imekuwa wenzo muhimu katika uhusiano wa kimataifa na diplomasia.

Na makala yetu ya wiki inafikia tamati hapa; tukutane tena juma lijalo panapo majaliwa yake Mola. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *