Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC jana Jumatatu ilimtia hatiani kiongozi wa kwanza wa wanamgambo wa Janjaweed aliyepandishwa kizimbani akihusishwa na ukatili na jinai zilizofanyika katika jimbo la Darfur nchini Sudan zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Mahakama hiyo imempata Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman na hatia kwenye makosa 27 ya uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na ubakaji, mauaji na mateso.

Hukumu dhidi ya ‘mbabe huyo wa kivita’ itaamuliwa baadaye, baada ya duru mpya ya kusikilizwa kwa faili lake, shirika la habari la Reuters limeripoti.

Hukumu dhidi yake katika kesi ya kwanza na ya pekee inayohusu uhalifu nchini Sudan tangu kesi hiyo kupelekwa mahakamani na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 2005, ni hatua kubwa ya kihistoria kwa ICC.

Mzozo wa Darfur kwa mara ya kwanza ulianza mwaka 2003 wakati waasi wengi wasio Waarabu walipoanzisha mashambulizi ya silaha dhidi ya serikali ya Sudan, wakiishutumu kwa kulitenga eneo hilo la mbali la magharibi mwa nchi.

Serikali ya wakati huo ya Sudan ilikusanya wanamgambo wengi wa Kiarabu, waliojulikana kama Janjaweed, ili kukomesha uasi huo, na kusababisha wimbi la ghasia ambazo mashirika ya kutetea haki za binadamu yalisema yalikuwa sawa na mauaji ya halaiki.

Jaji Kiongozi wa ICC, Joanna Korner amesema mahakama hiyo kwa kauli moja ilmemkuta Abd-Al-Rahman, ambaye pia anajulikana kwa jina la utani Ali Kushayb, na hatia ya makosa yote aliyokuwa ameshtakiwa nayo na akatupilia mbali utetezi wake kwamba alishtakiwa kimakosa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *