
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameonya kuwa, hatua zozote za makosa zitakazofanywa na maadui katika Ghuba ya Uajemi, Lango Bahari la Hormuz au katika visiwa vya Iran, zitakabiliwa na jibu kali na la kujutisha.
Meja Jenerali Mohammad Pakpour alisema hayo katika ujumbe wake kwa mnasaba wa Siku ya Jeshi la Wanamaji la IRGC iliyoadhimishwa jana Jumatano na kuongeza kuwa, “Mahesabu yoyote ghalati (ya maadui) katika Ghuba ya Uajemi, Lango Bahari la Hormuz, au katika visiwa vya Iran, yatakabiliwa na jibu la uhakika, la haraka, la kukandamiza na la kujutisha.
Aidha Pakpour amevitaja vikosi vya wanamaji vya IRGC kuwa ni ishara ya imani thabiti, msimamo wa kimuqawama wa kiakili na uwezo wa kuzuia, akibainisha kwamba chini ya uongozi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, vikosi hivyo vina nafasi muhimu katika kuhakikisha usalama wa Ghuba ya Uajemi na maji yanayoizunguka.
Meja Jenerali Mohammad Pakpour amesisitiza kuwa, Jeshi la Iran limejiandaa kikamilifu kutoa jibu thabiti na kali kwa chockochoko tarajiwa za maadui.
Kamanda huyo mkuu wa SEPAH amesema kuwa, “Kama vile vikosi vya jeshi viliupigisha magoti utawala wa Kizayuni na Marekani katika vita vya kutwishwa vya siku 12, ikiwa harakati yoyote itafanywa na maadui katika bahari na visiwa hivyo, vikosi vya Jeshi la Iran na Jeshi la IRGC vitajibu kwa nguvu zote.”
Vile vile ametaja ari ya juu ya majeshi na imani kubwa katika maadili ya Kiislamu kuwa sababu kuu ya nguvu ya wanajeshi wa Iran ambayo inawatia hofu zaidi maadui.