Waziri wa Madini, Anthony Peter Mavunde amezindua ujenzi wa mgodi wa madini ya Kinywe (Graphite) unaofanywa na kampuni ya Faru Graphite Corporation inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania (Hisa 16%) na Black Rock Mining Limited (Hisa 84%) ambayo ni hatua kubwa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya sekta ya madini nchini.

Waziri Mavunde akiwa katika eneo la Mahenge wilayani Ulanga mkoani Morogoro amesema uzinduzi huo ni kielelezo cha kasi mpya ya uendelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta ya madini kwa kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Mradi huu si uchimbaji wa rasilimali pekee, bali ni injini ya maendeleo itakayochochea ukuaji wa viwanda, biashara, ajira na ustawi wa jamii katika eneo la Mahenge kwa ujumla” amesema Waziri Mavunde.

Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, mradi wa Mahenge unatarajiwa kugharimu takribani dola za Marekani milioni 510 (Zaidi ya Shilingi Trilioni 1.3) na unatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 400 wakati wa ujenzi na zaidi ya ajira 900 za kudumu pindi mgodi utakapoanza uzalishaji kamili.

Mbali ya ajira hizo pia zaidi ya Watanzania 4,500 wanatarajiwa kunufaika kwa ajira za msimu zitakazochochewa kupitia mnyororo wa thamani wa wachuuzi, wakulima, wasambazaji wa bidhaa na watoa huduma.

Kupitia uchimbaji huo serikali inatarajia kupata mapato ya zaidi ya dola bilioni 3.2 (zaidi ya Shilingi Trilioni 7) katika kipindi cha uhai wa mgodi, kupitia kodi, tozo, gawio, na mrabaha wa madini.

Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya Faru Graphite Corporation, amesema Serikali kupitia ubia huu inalinda maslahi ya taifa, ikinufaika kupitia hisa, kodi, ajira na mzunguko wa fedha.

Naye Mwenyekiti wa Bodi na Mwakilishi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Faru na Blackrock Mining, Black Rock Mining Limited, Richard Crookes, amesema kampuni yake imejipanga kuhakikisha utekelezaji wa mradi unafuata viwango vya kimataifa vya usalama na uhifadhi wa mazingira, sambamba na kuwekeza katika teknolojia rafiki kwa mazingira na pia wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi yaliyopokea uwekezaji huo mkubwa Morogoro.

Imeandaliwa na @moseskwindi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *