
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo huko mjini Geneva, Uswisi, Mkuu wa Kitengo cha Masuala ya Kibinadamu wa UN Women, Sofia Calltorp, ametoa wito wa kuchukua hatua za haraka na tofauti kufuatia usitishwaji vita wa hivi karibuni.
Hali ya sasa: matumaini magumu na uchovu mkubwa
Calltorp ameanza kwa kunukuu maneno ya mwanamke mmoja, mwanafunzi wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 22 huko Gaza: “Tunatumai usitishwaji vita utadumu. Hatuwezi kusema tuko salama kabisa, lakini tunatumai hawatairudia tena zahma hii safari hii kwani hatuwezi kuvumilia tena.”
Amesema maneno hayo yanaakisi mchanganyiko wa matumaini hafifu, uchovu uliokithiri, na nguvu tulivu zinazojitokeza kutoka kwa wanawake wengi tangu kuanza kwa usitishwaji wa mapigano. Ingawa hatua hiyo imepunguza vita, haijamaliza mgogoro uliopo amesema.
Takwimu zinazoogopesha na mahitaji makubwa
Akizungumzia kiwango cha vita, Calltorp amebainisha kwamba kwa takribani miaka miwili, wanawake na wasichana huko Gaza wameuawa kwa kiwango cha takribani watu wawili kila saa, na kwamba idadi hii “itasumbua dhamira yetu ya pamoja kwa vizazi vijavyo.”
Amesisitiza kuwa mahitaji ya wanawake na wasichana bado yako juu sana:
- Wanawake na wasichana zaidi ya milioni moja wanahitaji msaada wa chakula.
- Karibu robo milioni wanahitaji msaada wa dharura wa lishe.
- Wanawake wengi wamefurushwa makwao takribani mara nne wakati wa vita, na sasa wanahitaji makazi kabla ya majira ya baridi.
- Kila familia moja kati ya saba huko Gaza inaongozwa na mwanamke, na wanahitaji msaada unaowafikia moja kwa moja ili kuweza kulisha watoto wao, kupata huduma za afya, na kujenga maisha upya.
Wito, wanawake kiini cha kujikwamua
Calltorp ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuyageuza matumaini yaliyotokana na usitishwaji wa mapigano kuwa hatua halisi za kuleta usalama, ukarabati, na haki kwa wanawake na wasichana.
”Wanawake na wasichana lazima wawe wasanifu wa ukarabati wa Gaza,” amesema. “Kila kiasi cha dola 1 inayowekezwa kwa wanawake, inazalisha faida ya dola 8 kwa jamii nzima.”
Ameeleza kuwa mashirika yanayoongozwa na wanawake yamekuwa yakifanya kazi dhidi ya mazingira magumu sana wakati wote wa vita, yakitoa huduma, ulinzi, na matumaini.
Ujumbe mkuu wa UN Women ni wazi:
- Kuhakikisha kila kifurushi cha chakula na kliniki inawafikia wanawake na wasichana kwa usalama na inakidhi mahitaji yao halisi.
- Kuyajumuisha mashirika ya wanawake katika majibu ya kibinadamu, ukarabati, na kazi za ujenzi mpya.
”Kila mwanamke anayejenga upya duka la kuoka mkate, kliniki, au chumba cha darasa, anajenga upya amani,” Calltorp amehitimisha. “Kama tuko kweli kuhusu matumaini, lazima tuyafanyie kazi. Kama tuko kweli kuhusu amani, lazima tuirejeshe kupitia wanawake. Na kama tuko kweli kuhusu ubinadamu wetu wa pamoja, lazima tufanye hivyo sasa.”
UN Women imetoa wito kwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuongeza ufadhili mara moja, ili kuwezesha upanuzi wa msaada wa kuokoa maisha Gaza.