
Katika maoni ya ushauri wa kina yaliyoombwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa imebaini kwamba Israeli inapaswa “kuhakikisha kuwa wakazi wa Ardhi ya Palestina Iliyokaliwa kwa Mabavu wanapata mahitaji muhimu ya maisha ya kila siku, ikiwemo chakula, maji, nguo, mashuka, makazi, mafuta, dawa na huduma za matibabu.”
Mahakama pia imeitaka Israeli “kuheshimu na kulinda” wafanyakazi wote wa misaada, wahudumu wa afya na vituo vyao.
Kwa kura kumi dhidi ya moja, majaji pia wamekubaliana kwamba Israeli “ina wajibu” wa kushirikiana kwa nia njema na Umoja wa Mataifa, “ikitoa msaada wote katika hatua zozote itakazochukua kwa mujibu wa Katiba ya Umoja wa Mataifa,” ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).
Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameelezea maoni hayo ya ICJ kuwa “muhimu sana,” akiongeza kuwa yametolewa wakati ambapo Umoja wa Mataifa unafanya kila juhudi kuongeza kasi ya misaada kuingia Gaza baada ya kusitishwa kwa mapigano.
Maoni hayo yaliyoombwa Desemba 2024 yanazungumzia wajibu wa Israeli katika uhusiano wake na Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika mengine ya kimataifa na nchi zinazohusika na shughuli za kibinadamu nchini Palestina.
Ili kuonesha kiwango cha ushiriki wa kimataifa katika kesi hiyo, mataifa na mashirika 45 yaliwasilisha taarifa kwa maandishi, na 39 yaliwasilisha hoja kwa maneno wakati wa vikao vilivyofanyika kuanzia tarehe 28 Aprili hadi 2 Mei 2025.
Umuhimu wa mahakama
Mahakama ya Kimataifa ya Haki, yenye makao yake mjini The Hague, ndiyo chombo kikuu cha kisheria cha Umoja wa Mataifa.
Inashughulikia migogoro ya kisheria kati ya mataifa na kutoa maoni ya ushauri kwa ombi la taasisi za Umoja wa Mataifa.
Ingawa maoni yake hayalazimishi kisheria, yana uzito mkubwa wa kimaadili na kisheria na mara nyingi huelekeza sera na mienendo ya kimataifa.
Kufuata sheria za kimataifa
ICJ imeeleza kuwa Israeli inawajibika chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu kuheshimu na kulinda raia katika Ardhi ya Palestina Iliyokaliwa kwa Mabavu, kuhakikisha kuwa wafanyakazi wa misaada na vituo vya afya vinalindwa, na kwamba hakuna raia anayehamishwa kwa nguvu au kunyimwa chakula.
Majaji kumi kati ya kumi na mmoja wamekubaliana kuwa Israeli lazima iheshimu hadhi na kinga za Umoja wa Mataifa na maafisa wake, kwa mujibu wa Katiba ya Umoja wa Mataifa. Hii inajumuisha “kutokuguswa” kwa majengo yote ya Umoja wa Mataifa yakiwemo yale yanayosimamiwa na UNRWA.
Makamu wa Rais wa mahakama, Jaji Julia Sebutinde kutoka Uganda, ndiye aliyepiga kura ya kupinga katika sehemu kadhaa.
Mahakama pia imesisitiza wajibu wa Israeli kuruhusu Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) kupata fursa ya kuwaona wafungwa katika Ardhi ya Palestina Iliyokaliwa kwa Mabavu na “kuheshimu marufuku ya kutumia njaa ya raia kama mbinu ya vita.”
Wizara ya Mambo ya Nje ya Israeli imesema kupitia mitandao ya kijamii kwamba “inakataa kabisa” maoni hayo ya ICJ, ikiyaeleza kama “jaribio jingine la kisiasa kulazimisha hatua za kisiasa dhidi ya Israeli.”