Sehemu ya 11

PICHA za Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake zilianza kujirudia akilini mwake. Ni kama alikuwa akijiona akitua kwenye Uwanja wa kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA).

Mbali na kuvuta picha akiwa anatua kwenye uwanja huo, pia ni kama alikuwa akiwaona askari waliokuwa wakimsubiri na kumfikisha mahakamni kukubaliana na kesi yake ya kumuibia Kamba Makambo.

Kulikuwa na kitu kingine ambacho kilikuwa kinamkatisha tamaa kabisa, Muddy alifahamu kuhusu tabia za wazungu huwa hawakosei pale wanapotaka kutimiza jambo lao.

“Kila kitu chao huwa kinaendeshwa kwa muda na utalaamu na kujali muda zaidi…” aliwaza.

Wasiwasi ulikuwa kuhusu wale maofisa wa uhamiaji waliomkata wangeweza kushughulikia suala lake haraka na kumrudisha Tanzania.

Muddy alifahamu asingeweza kutoboa kwa kukaa kwa muda mrefu katika chumba kile pasi na kurudishwa nyumbani.

Hivyo, akayafuta mawazo ya mwanamke aliyejitambulisha kwake kwa jina la Linnie Jonson kama angemkuta pindi atakaporudi kazini jioni.

Pamoja na kufahamu yote hayo lakini bado, Muddy alitamani miujiza itokee na kila kitu kichelewe na Linnie arudi jioni na kumkuta akiwa bado hazijachukuliwa hatua zozote za kumrudisha Tanzania.

Kuna kitu tofauti ambacho Muddy alikiona kwa mwanamke yule, alihisi labda Linnie ndiye angeweza kuwa mwokozi wake pekee aliyebaki kumuwezesha kutimiza ndoto zake za kuendelea na safari yake.

Kitu kilichokuwa kikimpa matumaini ni wakati wawili hao walipokuwa wakizungumza, Muddy aliweza kuyatazama macho ya Linnie kwa ufasaha na kuhisi yalikuwa yakizungumza kitu fulani ndani yake.

Katika mtazamo wake alihisi Linnie alikuwa na upendo na huruma tofauti na wale maafisa wa uhamiaji wanaume waliomkamata na kumuhoji kuhusu safari yake ya kwenda katika nchi ya Uholanzi.

Kufutia mtazamo huo, aliamini laiti kama angekamatwa na mwanamke huyo mambo yasingefikia hapo yalipokuwa yamefikia.

Hata kitendo cha kupewa chai, vitafunwa na maji ya kunywa na Linnie, kilimfanya Muddy kuamini kilikuwa ni cha kiungwana zaidi kufanywa kwake na mwanamke yule wa Kizungu. Matumaini yake makubwa yalibaki kwa Linnie.

Ni kipindi hicho ndicho Muddy alipojua kama kulikuwa na Mungu anayepaswa kuombwa ili mambo yaweze kwenda vizuri.

Baada ya kunywa chai na vitafunwa alivyopewa na Linnie na kuweka uzito na nguvu tumboni huku akipunguza ukali wa baridi mwilini mwake, muda mwingi alikuwa akiutumia kuomba Mungu ili muujiza utokee na aruhusiwe kuendelea na safari yake.

Kikubwa alichokuwa akikiomba ni mambo yasiende sawasawa na muda uende kwa kasi ili apate fursa ya kukutana na Linnie kwa mara nyingine.

Fikra zake zilimwambia mwanamke huyo alikuwa ni mmoja kati ya wafanyakazi wa idara ya uhamiaji katika nchi ya Sweden wenye utu na ubinaadamu katika mioyo yao.

Akiwa ametawaliwa na mawazo, uchovu wa kukaa sehemu moja na shibe ya chai nzito iliyoambatana na vitafunwa alivyopewa na Linnie, Muddy alijikuta akipitiwa na usingizi mzito.

Usingizini… aliota ndoto akiwa katika mazingira magumu, aliota akiwa katika gereza mojawapo la Tanzania akitumikia kifungo.

Ndoto ilimuonyesha akiwa amevaa mavazi ya wafungwa na alikuwa akisumbuliwa na maaskari wa magereza na manyapara waliokuwa wakimshurutisha kufanya kazi ngumu.

Muddy aliota akiwa anabishana na kuwagomea askari hao wa Jeshi la Magereza kufanya kazi ngumu na mmoja wao alichukua rungu na kumpiga nalo kichwani… akiwa anaugulia maumivu… ghafla Muddy alishtuka kutoka usingizini.

Mara baada ya kushtuka alijikuta palepale kwenye Uwanja wa Ndege wa Arlanda… aligeuka kila upande kutaka kuhakikisha kama ni kweli alikuwa bado hajarudishwa nyumbani…

Baada ya kutosheka na alichokiona alijiweka sawa na kuanza kuitafakari ndoto yake. Moja kwa moja aliamini alikuwa akionyeshwa hatma yake baada ya kutoka hapo. Alijua angerudishwa nyumbani Tanzania na kukutana na kesi yake ya kumuibia Kamba Makambo na angeswekwa gerezani.

“Nilikuwa naonyeshwa kitu ambacho nitaenda kukutana nacho nyumbani…” alijisema mwenyewe.

Hapo Muddy alipoteza matumaini kabisa ya kuendelea na safari yake ya Uholanzi. Aliamini Fashanu alikuwa amekosea kumchongea mchongo ambao usingekuwa na shaka kwa maafisa wale wa uhamiaji.

KWA upande wake Linnie tangu alipomuona Muddy alipokuwa akihojiwa na maofisa wenzake alivutiwa na tukio hilo na kutaka kujua kilichomsibu kijana huyo.

Kuna kitu kilikuwa kimemvutia kumwangalia abiria aliyeshikwa na maofisa uhamiaji wenzake na kuamini alipaswa kufuatilia tukio zima.

Mwanzo naye alikuwa na mtazamo hasi dhidi ya abiria huyo kutokana na mavazi aliyokuwa ameyavaa.

Pia, ni jinsi alivyokuwa akizungumza kwa wasiwasi na hata rangi yake ya ngozi ilichangia kumhukumu kwa sababu iliaminika vijana wengi wa Kiafrika wamekuwa wakitumika katika biashara haramu ya kusafirisha dawa za kulevya.

Hivyo, Linnie aliyafuatilia hatua kwa hatua mahojiano aliyokuwa akifanyiwa Muddy hadi alipobaini makosa yake alitafuta muda wa kukutana naye ili kuweza kupata undani wake.

Mbali na hivyo, kuna kitu kilimvutia, Linnie alijikuta akipata hamu ya kutaka kuzungumza na mtuhumiwa ili aweze kusikia, akafanya hivyo kisha akatoa ahadi yake ya kuweza kumsaidia.

Kikwazo kikubwa kilichomfanya asiweze kumsaidia wakati ule alipokuwa akizungumza naye ni muda wake wa kuwepo ofisini ulikuwa umeshaisha. Tayari alishamaliza zamu yake na nafasi yake ilishachukuliwa na mtu mwingine.

Linnie aliondoka na kumuacha Muddy akisubiri kurudishwa Tanzania. Alifahamu kama jambo hilo lingetimia basi hati yake ya kusafiria ingegongwa mhuri mwekundu na asingeweza tena kuitumika kuingia katika nchi yoyote katika Bara la Ulaya.

Kwa upande wake Muddy alikuwa akiuona muda ni kama hauendi kwa kasi iliyokuwa unaostahili na alihisi ulikuwa ukienda taratibu mno.

Ingawaje sehemu aliyokuwapo ilikuwa na viyoyozi vya kutosha lakini alihisi hali ya joto ikizidi kumtawala mwilini mwake kutokana na hofu, wasiwasi na woga wa kurudishwa Tanzania.

Fukuto la joto hilo alilisikia zaidi ndani ya moyo wake na kumfanya tumbo lake limcheze mara kwa mara kama mgonjwa aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi ya kipindupindu. Wasiwasi ulimtawala sehehemu kubwa ya akili yake na hofu ikachukua nafasi kubwa usoni pake.

Katika kipindi hiki alishapoteza kabisa matumaini ya kuendelea na safari yake ya Uholanzi. Nafsi yake ilianza kumsuta, alihisi matendo yake na uovu aliomfanyia Kamba Makambo pale Kariakoo kwa njia moja ama nyingine ulikuwa umemfikisha hapo.

Ndio, alikuwa anakumbuka kila kitu alichokifanya hadi kufika katika hatua hiyo ya kuzuiwa katika Uwanja wa Ndege wa Arlanda.

Uhalifu haulipi.Malipo ya ubaya ni aibu na malipo ni hapahapa duniani, ahera huenda hesabu.

Ni baadhi ya misemo ambayo ilipita kwa haraka akilini mwake na kumkatisha tamaa. Wakati akiwaza hayo, jua lilianza kuzama, aliutumia muda mwingi kuangaza huku na kule kama angeweza kumuona Linnie ambaye aliamini angeweza kumtoa katika dhahama hiyo iliyomkuta lakini hakufanikiwa kumuona wala kumsikia mwanamke huyo.

 Pamoja na kuwa katika hali hiyo Muddy aliendelea kumuomba Mungu kwa juhudi kubwa kutaka mwanamke huyo awahi kufika na kumuokoa katika dhahama iliyokuwa ikimkabili.

Mpaka giza lilipokuwa likichukua nafasi, Linnie hakuwa ametokea. Lakini ghafla mlango wa chumba hicho ulifunguliwa na macho ya Muddy akayapeleka mlangoni kuangalia ni nani aliyekuwa akiingia.

Hakuwa Linnie kama alivyotarajia au alivyotamani iwe, bali alimshuhudia afisa mwingine wa kiume akiiingia ndani ya chumba hicho.

Moyo wake ukapiga mara kadhaa, mwili wake ukaishiwa nguvu na kuhisi moja moja ilikuwa safari ya kurudishwa Tanzania. Laiti macho yake yangemuona Linnie angeamini safari ya ukombozi ilikuwa imefika lakini kwa kumuona afisa huyo akaamini ndoto aliyoiota akiwa katika gereza la Tanzania ilikuwa imetimia.

Hata afisa yule alipomsalimia, Muddy hakuitikia salamu yake kwa bashasha kama ambavyo angeweza kuitikia salamu ya Linnie.

Muddy alimwangalia kwa kukata tamaa na hata alipoamriwa kuinuka na kuongozana naye alifanya hivyo akiwa katika hali ya unyonge.

Mara baada ya kupokea muongozo kutoka kwa afisa wa uhamiaji, Muddy alijua maombi yake yalikuwa yamegonga mwamba, aliamini ndege ya kumrudisha Tanzania ilikuwa imeshapatikana na alikuwa akipelekwa kukamilishiwa taratibu za kurudishwa nyumbani.

Kitendo hicho kilimchanganya zaidi akili na kuondoa matumaini yake ya kuendelea na safari yake ya Uholanzi.

Katika hali hiyo, hakika Muddy alitahayari na kupoteza matumaini kabisa. Mwili wake ulikuwa mzito… akaanza kuhisi uchovu wa akili na machozi yakaanza kumchuruzika katika mashavu yake. 

Pamoja na kutotaka kurudi Tanzania kutokana na nia yake ya kutafuta maisha Ulaya, kikubwa kilichokuwa kikimtisha ni kesi yake ya wizi.

Alifahamu pindi akirudishwa angeikuta kesi hiyo ikiwa bado mbichi, hivyo angeweza kuhukumiwa kifungo cha muda mrefu jela.

Kwa hali ya unyonge, Muddy alimfuata afisa wa uhamiaji ambaye alimuongoza hadi katika ofisi nyingine iliyokuwa na watu wengi.

Inaendelea…

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *