
Hata hivyo, ripoti hiyo iliyotolewa leo Jumatano, tarehe 22 Oktoba 2025, imeonya kuwa kasi ya hatua zinazochukuliwa bado ni ndogo. UNEP imesisitiza kuwa dunia inapaswa kuongeza juhudi ili kupunguza ongezeko la joto duniani na kufikia Ahadi ya Kimataifa ya Methane (Global Methane Pledge) inayolenga kupunguza uzalishaji wa methane kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2030.
Ufuatiliaji wa methane wa kisasa kuleta mabadiliko
Kwa muda mrefu, juhudi za kupima na kufuatilia uzalishaji wa methane zimekuwa zikikadiria chini ya kiwango halisi cha gesi hiyo yenye nguvu kubwa ya kuongeza joto duniani. Toleo la tano la ripoti ya Kituo cha Ufuatiliaji wa Uzalishaji wa Methane Duniani (IMEO) la UNEP lenye kichwa “Kuangalia Methane: Kutoka Vipimo hadi Hatua” limeonesha kuwa wanachama wa Ushirikiano wa Methane wa Mafuta na Gesi 2.0 (OGMP 2.0) wataanza kufuatilia takribani theluthi moja ya uzalishaji wa methane kwa kutumia vipimo vya moja kwa moja kutoka shughuli za mafuta na gesi.
Majibu ya serikali na kampuni yaongezeka mara kumi
Ripoti hiyo pia imeonesha kuwa majibu kutoka kwa serikali na kampuni kwa tahadhari za mfumo wa Mfumo wa Tahadhari na Mwitikio wa Methane (MARS) yameongezeka zaidi ya mara kumi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Licha ya mafanikio hayo, karibu asilimia 90 ya tahadhari bado hazijapatiwa majibu, jambo linaloashiria hitaji la hatua za haraka zaidi.
Methane bado ni changamoto kubwa ya kimazingira
Methane inabakia kuwa gesi ya pili kwa ukubwa inayochangia ongezeko la joto duniani baada ya hewa ya ukaa, ikiwa na mchango wa takriban theluthi moja ya ongezeko hilo.
“Kupunguza uzalishaji wa methane kunaweza kusaidia kupunguza kasi ya ongezeko la joto duniani na kutoa muda muhimu wa kuchukua hatua zaidi. Lakini ni muhimu kuhakikisha kuwa maendeleo haya ya takwimu yanatafsiriwa kuwa hatua za kupunguza uzalishaji,” amesema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP.
Ameongeza kuwa, “Ili kufikia Malengo ya Mkataba wa Paris, maendeleo katika ufuatiliaji lazima yaende sambamba na hatua za kupunguza uzalishaji.”
Wito kwa kampuni na serikali kuchukua hatua za kweli
Bi. Andersen ametoa wito kwa kampuni zote kujiunga na OGMP 2.0, na kwa serikali pamoja na waendeshaji wa sekta ya mafuta na gesi kujibu kwa haraka tahadhari za satelaiti — na muhimu zaidi, kuchukua hatua za moja kwa moja kupunguza uzalishaji wa methane.