Akizungumza hii leo katika Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu Tahadhari za Mapema kwa Wote uliofanyika wakati wa Kikao Maalum cha Mkutano wa Hali ya Hewa Duniani mjini Geneva, amesema kazi ya WMO imegeuza takwimu kuwa uelewa, na uelewa huo kuwa “hatua za kuokoa maisha.”

“Bila uchambuzi na utabiri wenu makini, tusingejua nini kinakuja au jinsi ya kujiandaa,” amesema Guterres. “Wanasayansi na wataalamu wa hali ya hewa wa shirika lenu wanaishi kila siku kwa kauli mbiu ya Sayansi kwa ajili ya Hatua.’

Mgogoro wa tabianchi unasababisha majanga ya kihistoria

Katibu Mkuu ameonya kwamba ongezeko la joto duniani “linaisukuma sayari yetu ukingoni,” huku kila moja ya miaka kumi iliyopita ikiwa kati ya yenye joto zaidi katika historia.

Joto la bahari linavunja rekodi, linaangamiza mifumo ya ikolojia, na kuongeza mafuriko, moto wa nyika na dhoruba katika kila eneo. “Hakuna nchi iliyo salama,” amesema, akisisitiza kuwa maskini zaidi na walio hatarini hasa nchi ndogo za visiwa na nchi maskini zaidi ndio wanaobeba gharama kubwa zaidi.

“Ripoti zenu za Hali ya Tabianchi zinasimulia hadithi moja ya wazi. Kila moja ya miaka kumi iliyopita imekuwa yenye joto zaidi katika historia.” Amesema.

Tahadhari za mapema zinaokoa maisha na mali

Akionesha nguvu ya mifumo ya tahadhari za mapema, Guterres amesema nchi zenye mifumo thabiti zinapoteza watu wachache zaidi.

“Vifo vinavyosababishwa na majanga ni angalau mara sita chini katika nchi zenye mifumo bora ya tahadhari,” amesema, akiongeza kuwa hata saa 24 tu za onyo kabla ya tukio hatarishi zinaweza kupunguza uharibifu kwa hadi asilimia 30.

Amesifu mafanikio yaliyopatikana hadi sasa ambapo zaidi ya asilimia 60 ya nchi sasa zinaripoti kuwa na mifumo ya tahadhari inayoshughulikia hatari nyingi, huku nchi maskini zaidi zikiongeza uwezo wao karibu mara mbili tangu utoaji ripoti uanze rasmi.

Maendeleo katika teknolojia ya kidijitali na akili Mnemba amesema  yanaendelea kuboresha mfumo wa utabiri na uhamasishaji wa tahadhari.

Mpango wa UN wa “Tahadhari kwa wote kufikia 2027”

Guterres amekumbusha kuzinduliwa kwa mpango wa Tahadhari za Mapema kwa Wote mwaka 2022, unaolenga kuhakikisha kwamba “kila mtu, kila mahali analindwa na mfumo wa tahadhari ifikapo mwaka 2027”.

Amekaribisha Wito wa Kuchukua Hatua uliotolewa na Katibu Mkuu wa WMO wiki hii na kubainisha maeneo matatu ya hatua za haraka ambbayo ni “ kuingiza mifumo ya tahadhari katika sera za kitaifa, kuongeza ufadhili, na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, biashara na jamii kufikia walio hatarini zaidi.”

Amesema “Serikali lazima zijumuishe mifumo ya tahadhari katika sera, taasisi na bajeti zao. Hii ni kuhusu kuokoa maisha, si kukusanyatakwimu pekee.”

Ufadhili kwa mnepo na urekebishaji wa tabianchi

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba kufikia kila jamii kunahitaji “ongezeko kubwa la fedha.”

Ametaja makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano wa Ufadhili wa Maendeleo uliofanyika Seville mapema mwaka huu kuhusu kufungua rasilimali zaidi kwa nchi zinazoendelea, kupanua uwezo wa taasisi za kifedha za kimataifa, na kupunguza mzigo wa madeni.

Ameonya kwamba “Nchi nyingi zinazoendelea zimefungwa mikono na ukosefu wa nafasi ya kifedha, ukuaji mdogo wa uchumi, na madeni makubwa”.

Ametoa wito wa mageuzi katika taasisi za kifedha za kimataifa ili ziweze kuhudumia vyema mataifa yaliyo hatarini na kuzitaka nchi tajiri kutimiza ahadi zao za mara mbili ya ufadhili wa hatua za urekebishaji hadi angalau dola bilioni 40 mwaka huu.

Wito wa uadilifu wa tabianchi na nishati mbadala

Akiangazia kuelekea Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Umoja wa Mataifa (COP30) utakaofanyika Brazil, Guterres amezihimiza nchi zote kuwasilisha mipango mipya ya kitaifa inayolingana na lengo la kusalia na nyuzi joto 1.5°C, ikijumuisha malengo thabiti ya kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa katika muongo ujao.

Ametaka kuwe na mpango wa wazi wa kuhamasisha dola trilioni 1.3 kila mwaka kufikia mwaka 2035 kusaidia nchi zinazoendelea, na kusisitiza kuwa nishati mbadala “ndiyo chanzo cha bei nafuu, cha haraka na chenye busara zaidi.”

Ameonya pia kuhusu “upotoshaji wa taarifa, unyanyasaji mtandaoni na ujanja wa kujali mazingira,” akitangaza Mpango wa Uadilifu wa Taarifa za Tabianchi Duniani kulinda ukweli wa kisayansi.

“Wanasayansi hawapaswi kuogopa kusema ukweli,” amesema. “Nitasimama nanyi daima.”

Akimalizia hotuba yake, Guterres amethibitisha umuhimu wa WMO “Ninyi ndio nguvu tulivu nyuma ya kila uamuzi wa busara wa hali ya hewa tunaouchukua. Tuweke sayansi katika huduma ya hatua na haki ambayo watu na sayari yetu wanaihitaji kwa dharura.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *