Wakati Sudan Kusini inapokaribia kufungua ukurasa wake mpya wa kidemokrasia hapo Desemba mwaka 2026, vijana wa nchi hiyo wanajitokeza kwa ujasiri wanapaza sauti zao wakiwa na uelewa, msukumo na wako tayari kuongoza.
Tamba Isaiah, kijana mkazi wa kituo cha wakimbizi wa ndani, anasema awali hakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu uchaguzi.
“Hapo awali nilikuwa na mitazamo potofu kuhusu uchaguzi na sikuwa najua vizuri hatua zake, kuanzia kabla ya kupiga kura hadi baada ya uchaguzi, lakini leo mashaka yangu yote yameondoka.”
Tamba Isaiah, kijana mkazi wa kituo cha wakimbizi wa ndani nchini Sudan Kusini.
Kwa vijana wengi, hasa wanawake, ushiriki wao kabla na wakati wa uchaguzi ni muhimu sana, licha ya vikwazo vya kijamii na kitamaduni kama anavyoeleza Aluel Victoria mwakilishi wa vijana mjini Yambio
“Changamoto kubwa ni ubaguzi wa kijinsia upande wa wanawake, na sisi vijana tunaonekana hatuna uzoefu wa kutosha kushiriki kikamilifu,”
Wadau wa masuala ya kijamii wanasema iwapo kila mtu atashirikishwa na kupewa uhuru wa kushiriki kwa usalama, taifa hilo linaweza kupata umoja wa kweli. Michael Dakpari Peter ni mwakilishi wa mtandao wa asasi za kiraia.
“Hali ya usalama bado ni changamoto hasa kwa wanawake na watu wenye ulemavu. Tunahitaji mazingira salama ili wote waweze kushiriki ipasavyo.”
Tukitambua changamoto hizo, Tume ya Uchaguzi ya Jimbo la Equatoria Magharibi imetambua changamoto hizo na kuanzisha kampeni za kutoa elimu kwa umma kama anavyoeleza msemaji wa tume hiyo, Simon Sarawasi.
Simon Sarawasi – Mwihava
“Tumetoka ofisini na kwenda kwa wananchi kutoa elimu ya uchaguzi kwa sababu huu ni uchaguzi wa kwanza nchini Sudan Kusini. Vijana wengi wenye miaka wa miaka 18 na kuendelea hawajawahi kushiriki uchaguzi. Tunafanya kazi kwa karibu na timu ya Umoja wa Mataifa kusaidia kufikisha elimu hii kwa watu wote.”
Kampeni hizi zinaungwa mkono na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS, ambao unasaidia kuelimisha wananchi kuhusu haki na wajibu wao wa kiraia. Afisa wa haki za binadamu wa UNMISS, Opubo Melford, anasema
Opubo Melford – Evarist
“Tunafanya kazi kwa ushirikiano na idara mbalimbali kutoa elimu kwa jamii kupitia warsha zetu. Kila mara tunatenga muda kuzungumzia masuala ya uchaguzi, tukiwalenga pia maafisa wa polisi, majeshi na raia.”
Kadiri Desemba 2026 inavyokaribia, vijana wa Sudan Kusini wanajiandaa kuchukua nafasi yao katika kujenga mustakabali wa taifa lao katika uchaguzi wa kwanza wa kitaifa tangu uhuru wa taifa hilo mwaka tarehe 09 Julai 2011.