Katika mahojiano maalum yaliyofanywa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kwenye maeneo mbalimbali Afrika Mashariki wananchi na wadau wa asasi za kiraia wameeleza umuhimu mkubwa wa shirika hilo katika kusongesha malengo ya maendeleo endelevu, kushirikisha vijana katika maamuzi na kuchagiza amani
Wakimbizi
Uganda ni moja ya nchi zinazohifadhi wakimbizi wengi duniani hususan kutoka Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.
Katika viunga vya jiji la Hoima, John Kibego kutoka redio washirika wa Umoja wa Mataifa Kazi Njema FM amezungumza na vijana wanafunzi wa shule ya sekondari Geneva ambao pia ni wakimbizi kutoka nchini DRC.
Coletha Magreth binti mkimbizi ameishukuru Umoja wa Mataifa kwa kuwakaribisha Uganda “Umetupatia elimu kwani watu wengi hawajapata fursa hii ya kupata elimu tena ya hali ya juu”. Ameeleza kuwa wakimbizi wengi wanavyosaka hifadhi Umoja wa Mataifa huwasaidia kupata vitu vingi na kutunzwa vizuri kushindwa hata maeneo waliyotokea.
Naye Job Kabagaya ambaye ni Kiranja Mkuu katika shule ya Geneva Senior na mkimbizi wa DRC anayeishi katika kambi ya Kyangwali mjini Hoima amushukuru Umoja wa Mataifa kwa ile alichoeleza imempatia maisha baada ya kukimbia vita nchini mwake.
Kabagaya ameeleza namna shirika hilo linavyowasaidia watu mbalimbali vijana kwa wazee na kutoa ushauri wake wakati shirika hilo linapotimiza miaka 80. “Mambo ambayo yamefanywa na Umoja wa Mataifa ni mengi lakini kama unavyojua hakuna mazuri yasiyokosa mabaya na hakuna aliyekamilika duniani. Umoja wa Mataifa ningeomba kama mkimbizi, isiishie tu kwa kuwasaidia wakimbizi lakini katika mwaka wa 81 mnaoelekea muweze kuleta amani katika nchi zote ambazo zipo na vita.”
Ameongeza kuwa “Ukimbizi usiwe ndio mahali tu pa kusaidia, mlete amani katika nchi hizo maana nasi tunapenda kukaa katika nchi zetu. Tukipata nafasi ya kukaa katika nchi zetu mtakuwa mmetusaidia sana.”
Marynsia Mangu – Mwanzilishi wa taasisi ya Mikono yenye mafanikio
Asasi za kiraia
Mbali na masuala ya wakimbizi na ulinzi wa amani, kuna fursa mbalimbali kwa vijana kushiriki moja kwa moja na pia kujifunza jinsi maamuzi yanavyofanyika kwenye mikutano ya Umoja wa Mataifa.
Marynsia Mangu ni mmoja wa vijana ambaye amekuwa akihudhuria mikutano mingi ya Umoja wa Mataifa akiwakilisha taasisi anayoiongoza ya Success hands Tanzania Initiative.
Maynsia ameeleza namna vijana wanavyonufaika kwa kupewa nafasi ya kushiriki katika mikutano hiyo ya maamuzi akisema “vijana wanaleta sauti, ubunifu na mawazo tofauti ya kubadilisha kesho yetu”
Akituma ujumbe kwa vijana amewakumbusha kuwa ‘Umoja wetu ndio nguvu yetu na kila mmoja wetu ana jukumu katika kujenga Dunia tunayo tamani iwe kwa kulinda mazingira, kusaidia mtoto kupata elimu, na kusimama kwa haki na amani.”
Na kwa vijana akawa na ujumbe mahususi “wito wangu kwa vijana tusisubiri nafasi, bali tuziumbe, tusisubiri mabadiliko bali tuyafanye, sisis ndio kizazi cha mabadiliko, sisi ndio Umoja wa Mataifa.”
Peter Omondi (kati), Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Global Youth Forum linalounganisha vijana Kenya, akiwa na vijana wachezaji wa mpira wa miguu.
Maendeleo endelevu SDGs
Huko nchini Kenya mwanaharakati Omondi Peter ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Global Youth Forum linalojihusisha na kusongesha malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa SDGs kupitia mpira wa miguu au kabumbu ambaye anashirikiana bega kwa bega na Umoja wa Mataifa kushirikisha vijana katika malengo hayo ameeleza kwake Umoja wa Mataifa unamaanisha mambo makuu matatu
“Mosi, kudumisha amani duniani. Pili, kuendeleza maendeleo endelevu na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma na tatu, kuleta wadhamini mbalimbali kuhakikisha nchi zote zinazokumbwa na majanga zinasaidiwa kutatua shida zao.”
Ametoa wito kwa vijana nchini Kenya, barani Afrika na Dunia kwa ujumla akiwa ameushikilia mpira wa miguu uliochorwa namba na kuwekwa malengo 17 ya SDGs “Kama vile paneli 32 zilivyotumika kuunda mpira huu tunaweza kuungana na tusaidie Umoja wa Mataifa kutekeleza maendeleo endelevu na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma. Heri ya siku ya Umoja wa Mataifa, kama kijana usikubali kuachwa nyuma kwenye utekelezaji wa maendeleo endelevu.”