
Mawakili wa Waziri Mkuu wa zamani wa Chad na kiongozi wa upinzani aneyezuiliwa jela Succès Masra waliwasilisha ombi la kuachiliwa kwa muda kwa mteja wao mnamo Oktoba 13, 2025, kwa sababu za kimatibabu. Pia waliomba ruhusa ya kuondoka nchini ili aweze kupata matibabu nje ya nchi: maombi haya hayajajibiwa.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu huko N’Djamena, Nadia Ben Mahfoudh
Waziri Mkuu wa zamani wa Chad na kiongozi wa upinzani Succès Masra anaripotiwa kuwa na matatizo kadhaa ya kiafya, hasa matatizo makubwa ya kupumua. Daktari wake anapendekeza aachiliwe ili aweze kupata huduma ya kutosha ya kimatibabu, lakini anaonyesha kuwa huduma inayofaa haipatikani nchini Chad.
Kulingana na Katibu Mkuu wa chama cha Transformateurs, Dkt. Tog-Yeum Nagorngar, matatizo haya ya kupumua yanaanzia mwaka 2019 na kutangazwa kwa kuundwa kwa chama hicho. Inaonekana zilisababishwa na gesi ya kutoa machozi, anaeleza, kabla ya kuongeza kwamba matatizo mapya ya kiafya yameibuka tangu kukamatwa kwa Succès Masra mnamo Mei 16, 2025.
Kulingana na serikali, afya yake “haihitaji kuhamishwa”
Kisha swali linaibuka kuhusu maingira ambamo anazuiliwa Waziri Mkuu wa zamani. Bw. Ouande, mmoja wa mawakili wake, anaeleza kwamba “anashikiliwa katika ofisi ya zamani iliyobadilishwa kuwa chumba cha jela.” Anabainisha kwamba Succès Masra anapewa huduma kadhaa kama vile kuoga na haja zingine, lakini kwamba analala “kwenye blanketi sakafuni.” Kinachoongezwa kwa hili ni “kutengwa,” anongeza.
Lakini kulingana na Gassim Cherif, Waziri wa Mawasiliano na msemaji wa serikali, Succès Masra “anashikiliwa katika mazingira mazuri zaidi nchini Chad.” Anaongeza kuwa “vipimo vya pili vya kimatibabu” vimehitimisha kwamba “hali ya afya ya Succès Masra haihitaji kuhamishwa.” Kwa upande wake, Bw. Ouande anabainisha kwamba upande wa utetezi haukujua kuhusu vipimo hivi vya pili.
Succès Masra alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela mnamo Agosti 9, 2025, na kulipa faranga za CFA bilioni 1 (euro milioni 1.52) kama fidia kwa kusambaza jumbe za chuki na ubaguzi na kushiriki katika mauaji katika kesi ya Mandakao. Mauaji ya halaiki yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya arobaini katika kijiji kimoja kusini mwa nchi, siku mbili kabla ya kiongozi huyo wa upinzani kukamatwa.