Wanaharakati wawili raia wa Kenya ambao walikuwa wametoweka wakati wakihudhuria mkutano wa kisiasa wa mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, wamechiwa huru.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Taarifa ya kuachiwa huru kwa wawili hao ilithibitishwa na wanasheria pamoja na mashirika ya kutetea haki za bindamu Jumamosi ya wiki hii.
Bob Njagi na Nicholas Oyoo walitoweka mwezi Oktoba baada yao kusafiri kwenda nchini Uganda kumuunga mkono kiongozi wa upinzani Bobi Wine, ambaye analenga kupambana dhidi ya Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Kupitia taarifa fupi kwenye mtandao wa X, mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty Kenya, Vocal Africa pamoja na chama cha wanasheria wa Kenya (LSK) yalikaribisha kuachiwakwa wanaharakati hao Nicholas Oyoo na Bob Njagi.
Wawili hao waliachiwa katika eneo la Busia, mpaka wa Kenya na Uganda baada ya kutoweka kwa siku 38.
Wawaili hao walitoweka mwezi uliopita, polisi nchini Uganda ikikanusha ripoti kuwa ilikuwa inawazuilia kwenye magereza yake.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya pamoja na familia za wanaharakati hao zimekuwa zikishinikiza serikali za Nairobi na Kampala kuhakikisha wawili hao wanaachiwa huru.
Mwezi uliopita, Kiongozi wa shirika la kutetea haki za binadamu nchini Kenya la VOCAL Africa, Hussein Khalid, alisema kwamba mashuhuda waliripoti kuwa watu waliokuwa wamefunika nyuso zao ambao pia walikuwa wamejihami waliwachukua raia hao wa Kenya.

Kulingana na Hussein Khalid matukio hao yalionyesha ishara kwamba serikali ya Uganda ilihusika na utekaji wa wanaharakati hao.
Wakosoaji na wapinzani wa serikali za Afrika Mashariki wamekuwa wakiripotiwa kutekwa na kuzuiliwa katika maeneo yasiojulikana kabla ya kuachiwa baadaye.
Mwezi Mei, mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi na mwenzake wa Uganda Agather Atuhaire waliripoti kutekwa na kuteswa na polisi nchini Tanzania.