Arusha. Kwa mara ya kwanza, Jiji la Arusha linatarajiwa kuandaa Mkutano Mkuu wa mwisho wa mwaka wa kimataifa unaohusu ukuaji wa akili Unde (AI) na mabadiliko ya kidijitali-Africa Premier AI Conference (APAIC 2025) katika Bara la Afrika.

Mkutano huo umepangwa kufanyika kuanzia Novemba 24 hadi 27 ukiangazia nafasi ya akili Unde hasa jinsi inavyoweza kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi barani Afrika na unatarajiwa kuvutia zaidi ya wajumbe zaidi ya 1,200, wataalamu watakaozungumza 150 na washiriki kutoka zaidi ya nchi 40.

Mkutano huo utaangazia mapinduzi ya akili Unde yenye uwezo wa Kujitegemea (Agentic AI) yanayounda mustakabali wa ubunifu, uhuru na uwezo wa binadamu.’ yakilennga mifumo ya akili Unde yenye uwezo wa kufikiri, kuchukua hatua na kujifunza yenyewe bila kutegemea binadamu moja kwa moja na jinsi mifumo hiyo inaweza kuendesha ukuaji na ujumuishaji wa Afrika.

Tofauti na matukio yaliyopita, APAIC 2025 inalenga kuhamia kutoka kwenye majadiliano kwenda kwenye utekelezaji kwa kuwaleta pamoja viongozi wa serikali, wavumbuzi, wawekezaji na wataalamu wa teknolojia ili kuunda mifumo ya vitendo ya matumizi ya akili Unde yenye maadili na jumuishi katika sekta kama afya, elimu, biashara, kilimo na utawala.

Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa APAIC 2025, Abdulwahid Ali Khamis amesema Afrika ipo katika hatua muhimu sana.

“Tunaweza ama kuendelea kuwa watumiaji tu wa teknolojia au tukawa wabunifu wa mifumo ya akili Unde inayodhihirisha maadili na vipaumbele vyetu. APAIC 2025 huko Arusha ndiko mabadiliko hayo yanapoanza.”

Mkutano huo umeandaliwa na ScanCode Tanzania, HAM International, pamoja na wadau wa kimataifa wakiwemo MindHYVE.ai (Marekani) inayoongozwa na mbunifu mashuhuri wa AI, Bill Faruki.

Wakiwa pamoja na mashirika ya maendeleo ya kikanda na vikundi vya sekta mbalimbali, wanatengeneza ramani ya bara zima (continental roadmap) kwa ajili ya elimu, ubunifu na utawala wa AI barani Afrika.

Moja ya mambo muhimu yatakayojitokeza kwenye mkutano huo ni uzinduzi wa The Dawn Directive mfumo wa kwanza duniani wa kujenga uelewa na umahiri wa AI (AI literacy and fluency framework) ambao umetengenezwa kwa ushirikiano na mfumo wa Agentic AI.

Mwongozo huu utasaidia watunga sera, wataalamu, na taasisi za elimu katika masuala ya elimu ya AI, maadili na ubunifu.

Pia alisema wajumbe wataona utiaji saini wa Azimio la Mombasa la Agentic AI linaloweka dira ya pamoja ya Afrika kuhusu utawala wa AI, matumizi ya kimaadili ya data na uwekezaji endelevu katika teknolojia.

Tukio hili litawaleta pamoja mawaziri, wakuu wa kampuni za teknolojia, wawekezaji, waanzilishi, wasomi na wanaharakati wa asasi za kiraia, wote wakihamasisha AI yenye maadili.

Anthony Nivo, Mkurugenzi wa Mkutano amesema: “AI si teknolojia ya siku zijazo tu, tayari ipo hapa sasa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *