
Mchezo wa riadha ni moja ya michezo yenye mashabiki wengi nchini Tanzania, utafiti unaonyesha kuwa baada ya soka na ndondi, riadha ndio mchezo wenye mashabiki wengi zaidi.
Manyara na maeneo ya jirani na mkoa huo, yanatajwa kuwa na nguvu kubwa ya kutoa wanariadha wengi na ni chimbuko la vipaji vya riadha hapa nchini tangu enzi za Gidamis Shahanga, Zakaria Barie na Juma Ikangaa waliotangaza taifa kimataifa miaka ya 1980, na sasa wapo Gabriel Geay, Magdelena Shauri na wengine.
Ni mkoa uliowahi kutikisha na mashindano makubwa ya dunia, na bado inaendelea kufanya vizuri, hususan kupitia wanariadha waliotoka vijijini lakini wakapanda majukwa ya dunia wakiwa wamebeba bendera ya Tanzania.
Sasa jina lingine kubwa kutoka mkoani humo, Mchungaji Zakayo Marekwa, ameliamsha tena jina la Manyara kupitia mchezo ulioifanya Tanzania ipate heshima kubwa miaka ya nyuma, kurusha mkuki (Javelin).
Marekwa si jina geni katika ulimwengu wa riadha, ni mwanariadha wa zamani wa kimataifa ambaye aliwahi kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya Afrika na Jumuiya ya Madola.
Mafanikio yake makubwa zaidi yalikuja mwaka 1982 huko Brisbane, Australia, aliporusha mkuki kwa urefu wa 78.46 mita, na kushinda medali ya fedha kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola.
Kupitia mafanikio hayo, Marekwa alipata ufadhili wa masomo nchini Marekani kwa miaka minne, huko alikua sio tu kielemu bali pia kimchezo, akijifunza falsafa ya uongozi na maadili ambayo leo yamekuwa msingi wa maono yake mapya.
Baada ya kustaafu, ameona haja ya kurudisha kwa jamii kile alichokipata, kwa moyo wa uzalendo na upendo kwa vijana wa nyumbani, ameanzisha Klabu ya riadha iitwayo Mashahidi Athletics Club, iliyopo Dongobesh, wilayani Mbulu, Mkoa wa Manyara.
Klabu hiyo inalenga kuibua na kulea vipaji vya vijana vya riadha, hususan katika michezo ya kurusha mkuki, kwani ni mchezo alioupenda na kuutumikia kwa mafanikio makubwa.
Lengo kufufua riadha
Akizungumza na Mwananchi, Mchungaji Marekwa anasema wazo hilo limetokana na kuona mchezo wa kurusha mkuki nchini umedorora, huku vijana wengi wakipoteza matumaini ya kuwa wanariadha wa kimataifa.
“Ni mchezo rahisi lakini unahitaji mbinu, mazoezi na nidhamu, nikiwaona wanariadha wa Kenya wakishinda kwenye runinga najihisi vibaya, mbona sisi Watanzania hatuwezi? Tuna nguvu, tuna ugali, tuna ari”.
“Hivyo nikaamua kuanzisha hii klabu ili kuonyesha kwamba inawezekana,” anasema Marekwa.
Anasema lengo la kuanzisha Klabu hiyo ni kufufua mchezo wa kurusha mkuki, hasa katika Mkoa wa Manyara unaotambulika kwa kutoa wanariadha bora wa muda mrefu.
“Manyara ni ardhi ya vipaji.Tunapaswa kuirudisha heshima ya michezo ambayo iliwahi kuanzia hapa na kuiwakilisha nchi kimataifa,” anaongeza.
Kuvumbua vipaji
Kwa mujibu wa Marekwa, Klabu yake hiyo ambayo imezunduliwa mwezi Oktoba mwaka huu, ina mpango kabambe wa kutambua na kulea vipaji, na wataanza kufuatilia vijana waliovutia siku ya uzinduzi wa klabu hiyo, wakishirikiana na viongozi wa vijiji, shule na wazazi.
“Tulipowaona siku ya ufunguzi walitupa matumaini. Tutawafuata hadi majumbani kwao, tukae na wazazi wao, tuwasajili rasmi, kwani tunataka kuandaa kizazi kipya cha wazalishaji wa mkuki”.
Aidha, wanapanga kuandaa mashindano ya kuibua vipaji pia watashirikiana na idara za elimu na michezo kwa lengo la kuwatambua mapema vijana wenye uwezo mkubwa kupitia mashindano ya michezo kwa shule za sekondari na msingi, hili kuwapa mwongozo wa kitaaluma kupitia klabu hiyo.
Apata sapoti
Jitihada za Mchungaji Marekwa hazijabaki bure. Serikali kupitia viongozi wa wilaya imempa sapoti kubwa, ishara kuwa maono yake yamepokelewa kwa mikono miwili.
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Semindu anasema kuanzishwa kwa klabu hiyo ni hatua muhimu ya kuinua vijana kupitia michezo, na ameahidi kuwa bega kwa bega kwa bega naye kuhakikisha vipaji vipya vinajitokeza.
“Klabu hii itakuwa chachu ya mafanikio, tutashirikiana kuhakikisha tunavumbua vipaji vingi vitakavyotangaza nchi kimataifa”.
“Tutaunda programu maalum ya kutambua vipaji, kuwalea na kuwajengea mazingira ya kambi bora Mbulu, tunataka heshima ya Mbulu irudi si kuhama kwenda mikoa mingine”.
“Vipaji tunavyo, nguvu tunao na sababu ya kushinda tunayo, leo tunaanza safari ya kurudisha wilaya ya Mbulu kwenye ramani ya michezo Tanzania”.
Arnd Weil na mke wake Simone ni wadau wa mchezo wa riadha kutoka nchini Ujerumani wakiwa na taasisi inayoitwa Bridge of Hope, wakiwa ni miongoni mwa watu ambao wamemsaidia Mchungaji Marekwa kufungua klabu hiyo ya mchezo wa riadha pia kuchangia vifaa mbalimbali ikiwemo mikuki.
Walionyesha kufurahishwa na juhudi mbalimbali ambazo zilionyeshwa na vijana ambao walishiriki mbio mbalimbali za viwanjani lakini pia kwenye miruko na mitupo ambapo wanaamini kupitia klabu hiyo sasa vijana watakwenda kutimiza ndoto zao kupitia mchezo wa riadha.
“Nimefurahishwa na viwango vya wanafunzi hapa, kwa kweli mwanga umeonekana na naamini vijana hawa miaka ijayo ndio wataleta medali nyingi kwenye mashindano makubwa ikiwemo Olimpiki”, alisema Weil.
RT yatia neno
Mjumbe wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Alfredo Shahanga, ambaye pia ni mshindi wa zamani wa Berlin Marathon, anatoa pongezi kwa Mchungaji Marekwa.
“Tunampongeza sana kwa uamuzi huu wa busara, kuanzishwa kwa klabu hii kunamaanisha vijana wengi kuingia kwenye mchezo wa kurusha mkuki”.
“RT tupo tayari kushirikiana naye kuhakikisha Manyara inatoa mabingwa wapya wa Afrika”.
Mwaka mpya Manyara
Kwa Manyara, hii ni kama Mwanga mpya wa michezo, Mchungaji Marekwa ameonesha mfano wa namna wanamichezo wastaafu wanavyoweza kuwa sehemu ya suluhisho badala ya kulalamika.
Kwa sasa, zaidi ya vijana 50 wanatazamiwa kusajiliwa katika klabu hiyo, wengi wao wakitarajiwa kutoka vijiji vya Dongobesh, Haydom na Bashay, ambapo watapewa mafunzo ya awali ya mazoezi, lishe bora, nidhamu ya mazoezi na mbinu za kiufundi za urushaji wa mkuki na michezo mingine ya riadha.
Licha ya changamoto za vifaa na miundombinu, Marekwa anaamini mwanzo ni nusu ya safari.
“Hatutegemei miujiza, tunategemea bidii, tukiwa na moyo wa uzalendo, tutafika, ninaamini mtoto wa Manyara atashika mkuki wa dhahabu kwenye mashindano ya kimataifa siku moja kama nilivyofanya mimi”.