
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine anazisihi serikali za Afrika kupambana na uajiri wa mamluki kupigana katika safu za jeshi la Urusi. Siku ya Ijumaa, Novemba 7, Andrii Sybiha alitoa wito kwa viongozi wa bara hilo kwenye mtandao wa kijamii wa X. Kulingana naye, angalau Waafrika 1,400 wa mataifa 36 tofauti wanapigana nchini Ukraine kwa niaba ya Moscow.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kulingana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, mamluki 1,436 wa Kiafrika wametambuliwa ndani ya jeshi la Urusi kwenye mstari wa mbele. Lakini idadi halisi inaweza kuwa kubwa zaidi, aliongeza. Kwa hivyo, Andrii Sybiha anaziomba serikali za bara hilo kutoa taarifa za umma kuwaonya raia wao. “Hatima ya raia wa kigeni katika jeshi la Urusi ni ya kusikitisha,” aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X. Wengi hutumwa katika maeneo “mabaya zaidi” ya mapigano, hutendewa “kama chakula cha mizinga,” na “hawaishi zaidi ya mwezi mmoja.”
Andrii Sybiha anadai kwamba waajiriwa huvutiwa na ahadi zenye faida, au kwamba hawajui ni kwa nini wanajiandikisha. Waziri huyo anawataka wale ambao tayari wako kwenye uwanja huo “kutumia kila fursa ya kutoroka” na kujisalimisha, akisema kwamba “kuwa mfungwa nchini Ukraine ni nafasi ya kutoroka na kurudi nyumbani.”
Kyiv inakabiliwa na ufanisi wa mawasiliano ya Urusi barani Afrika Kulingana na Jenerali Pellistrandi, mhariri mkuu wa Jarida la National Defense, wapiganaji 1,400 wa Kiafrika katika safu ya jeshi la Urusi ni idadi ndogo sana. “Mamluki wa Kiafrika waliotumwa upande wa Urusi hawaongezi thamani kubwa,” anasema, na kauli za waziri wa Ukraine “zinahusu zaidi mawasiliano kuliko mkakati wa kijeshi.”
Kwa upande mwingine, Kyiv inaweza kuweka msisitizo zaidi kwa mataifa 36 yaliyowakilishwa ndani ya kikosi hiki na juu ya “udanganyifu” wa Moscow kwa wanajeshi hawa. Kulingana na mtaalamu huyo, hii itasaidia kuwasilisha kwa ufanisi zaidi ujumbe wa kisiasa wa Ukraine wa kukabiliana na propaganda za Urusi katika bara la Afrika.
Miito ya kuomba msaada kutoka kwa raia wa Afrika Kusini wanaopigana nchini Ukraine
Uwepo wa wapiganaji wa Kiafrika nchini Ukraine chini ya bendera ya Urusi umeibuka tena katika habari nchini Afrika Kusini. Siku ya Alhamisi, Novemba 6, serikali ya Afrika Kusini iliripoti kupokea simu za dhiki kutoka kwa raia 17 ambao walikuwa wamejiunga na safu ya mamluki wa jeshi la Urusi na walikuwa wakiomba kurejeshwa nyumbani. Kulingana na taarifa kutoka ofisi ya rais, watu hao, wenye umri wa kati ya miaka 20 na 39, “walishawishiwa kwa mikataba mikubwa ya kujiunga na vikosi vya mamluki vilivyohusika katika vita kati ya Ukraine na Urusi,” bila kuambiwa ni upande gani wangepigania.
Waafrika Kusini hawa 17 “wamekwama katika jimbo la Donbas inayokumbwa na vita” na wanaomba “msaada wa kurudi nyumbani,” taarifa hiyo iliongeza. Rais Cyril Ramaphosa ameamuru uchunguzi ufanyike. Sheria ya Afrika Kusini inakataza kujiunga na jeshi la kigeni bila idhini ya serikali.