Kaveh Zahedi ambaye ni Mkurugenzi wa Ofisi ya Mabadiliko ya Tabianchi, Bioanuai na Mazingira, wa FAO akizungumza na idhaa ya Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa athari tabianchi kwa wananchi zipo wazi na kutaka juhudi za makusudi za kufanya uwekezaji wa kutosha katika mifumo ya chakula ili kujengea wakulima uwezo na ustahimilivu na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Zahedi amesema “Sio kwa siku zijazo. Inatokea hivi sasa. Hali mbaya ya hewa inaathiri chakula na kilimo leo. Inapunguza mavuno. Kutotabirika kwa hali ya hewa kunafanya iwe vigumu kwa wakulima kuvuna. Tukio moja kali linadhoofisha mavuno yote.”

Asemayo yamedhihirika kuanzia mafuriko huko Iran na Afghanistan, kimbunga katika nchi za Karibea mpaka ukame barani Afrika na wakuu wa nchi na serikali pamoja na wadau wanapokutana lazima waje na suluhu kusaidia wakulima.

“Ikiwa hatutafanya chochote kuhusu hilo, ikiwa mwelekeo utaendelea, hali ni kwamba katika baadhi ya maeneo ya dunia, haitawezekana kuwa na kilimo cha kulisha watu kinachotegemea mvua. Katika maeneo mengine ya dunia, uharibifu wa ardhi utaongezeka. Tayari tunayo theluthi moja ya ardhi ya kilimo ya kimataifa ambayo imeharibiwa. Embu fikiria kama hali hiyo itaongezeka. Kwa hivyo, yote haya, yanaweka shinikizo kwenye majukumu yetu, lakini mwishowe yanaweka shinikizo kwenye jamii zetu, mifumo yetu ya chakula na sisi pia.”

Kama wakulima wa viazi, familia ya Salma ilijiunga na Ushirika wa "Mkulima wa Birahim", ambao ulipata usaidizi muhimu katika kupanua upatikanaji wao wa fedha, masoko, teknolojia na habari.

© FAO/Saikat Mojumder

Kama wakulima wa viazi, familia ya Salma ilijiunga na Ushirika wa “Mkulima wa Birahim”, ambao ulipata usaidizi muhimu katika kupanua upatikanaji wao wa fedha, masoko, teknolojia na habari.

FAO inaposema “mifumo ya chakula”, inamaanisha mnyororo mzima unaohusisha jinsi chakula kinavyozalishwa, kusafirishwa, kuuzwa, kupikwa hadi kuliwa, kwahiyo hapa wakulima, masoko, watumiaji na mazingira yoote yanaunganishwa.

Katika COP wadau wote muhimu hususan watunga sera wanakuwepo na FAO inasema huu ni wakati mujarabu.“COP30 ni wakati muhimu sana kwa sababu nadhani ni wakati wa kusisitiza tena jinsi kilimo na mifumo ya chakula inapaswa kuwa sehemu muhimu ya majadiliano kuhusu mambo mbalimbali kama vile kuhusu kukabiliana na hali na kujenga ustahimilivu, kuhusu hasara na uharibifu, kuhusu fedha na wapi fedha hizo zinapaswa kuelekezwa katika kipindi cha mpito.Yote haya lazima, kwa njia moja au nyingine, yaguse kilimo, kwa maana hiyo, nikwamba yatagusa mifumo ya chakula kwa wakulima.”

Kisima kinachotumia nishati ya jua katika jamii ya Ipanama nchini Kolombia, husaidia wakulima kudumisha mazao katika maeneo ambayo yameathiriwa sana na mabadiliko ya tabianchi.

© FAO/Felipe Rodriguez

Kisima kinachotumia nishati ya jua katika jamii ya Ipanama nchini Kolombia, husaidia wakulima kudumisha mazao katika maeneo ambayo yameathiriwa sana na mabadiliko ya tabianchi.

Zahedi pia amesisitiza umuhimu wakujumisha wanajamii hususan jamii za asili katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kwa kipekee mkutano wa Tabianchi mwaka huu unafanyika mjini Belém, Brazil kwenye lango kuu la kuingia kwenye Msitu wa Amazon.

“Hauwezi kushughulika na misitu, hauwezi kushughulika na kilimo bila kushughulika na watu ambao hasa ndio walinzi wa hiyo ardhi, ambao wanazalisha chakula chetu, ndio wanaohusika na kilimo chetu. Na katika hali nyingi, hususani katika suala la misitu, ambayo wanaohusika kuitunza ni jamii za asili na ndio hasa wanaleta maarifa yao, maarifa ya jadi ambayo yanaweza kutulinda dhidi ya mustakabali usio na uhakika.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *