Afrika Kusini. Macho ya lejendari wa filamu, mchekeshaji na mwanamuziki, Joel Mafela (marehemu) yalijikuta yanavutiwa na mwanamke mmoja raia wa Kongo, akashawishika kumuandika wimbo kuonyesha mapenzi yake.
Mafela mzaliwa wa Afrika Kusini, Juni 25, 1943 katika mitaa ya Soweto na kufariki Machi 18, 2017. Katika albamu ya Shebeleza Felas aliyoitoa mwaka 1995, wimbo wa Okongo Mame Shebeleza ulimhusu mwanamke wake na unapendwa hadi sasa.
Wimbo huo si kwamba unawavutia watu wa kale pekee, bali hata Gen Z wanaukubali, hata kwa wale ambao hawajui maana yake, hivyo Mwananchi linakuchambulia una maana gani.
Kutokana na wimbo wa Okongo Mame Shebeleza, wengi waliamini kama Mafela ni raia wa Kongo, lakini ukweli wa mambo ni mtu wa Afrika Kusini, isipokuwa mwanamke wake ndiye alikuwa Mkongomani.
Neno Shebeleza kwa Kizulu linamanisha kucheza, akimaanisha mwanamke wake acheze kwa miondoko ya Kiafrika na katika video yake anaonekana akicheza na watoto.
Kwa maana hiyo, wimbo huo ni wa mapenzi unaweza ukatumika na mwanaume yeyote anayetaka kupeleka ujumbe kwa mpenzi wake, alitumia ubunifu mkubwa, kwani wakati mwingine mdundo wake unaweza ukadhani ni wimbo wa ukombozi.
Ukiachana na wimbo huo nyimbo zake nyingine ni Ekuseni, Jabula, Siyaya E France, Thoko, Mwambe hizo ni baadhi tu kati ya zilizowahi kutamba enzi zake.
Mafela anatajwa alikuwa mnyenyekevu na vipaji vingi kama mtayarishaji na muongozaji na nyimbo zake nyingi zilikuwa ni kuileta jamii kwa pamoja na ukombozi, jambo lililofanya apendwe na kupata umaarufu mkubwa barani Afrika.
Wikipedia inamuelezea Mafela alianza kazi ya uigizaji akiwa na umri wa miaka 22, ukiacha hilo aliandika filamu ya Real News, jambo lililozidi kumpa umaarufu mkubwa zaidi Afrika.
Alijiunga na kampuni ya Filamu ya Afrika Kusini (SA Films) pia alisimamia vikundi vya kucheza muziki kama Mzumba, Sangoma na kadhalika, pia aliwahi kuchukua tuzo mbalimbali za muziki na uigizaji.
Kinachozungumziwa ni sanaa yake ya kuufikisha ujumbe kwa mashabiki wake, vinginevyo wapo wasanii wengi ambao wamewaimbia wapenzi wao nyimbo za kuonyesha mapenzi yao.
Miongoni mwa hao ni marahemu Kikumbi Mwanzo Mpango ‘King Kiki’ aliwahi kumuimbia mkewe Clecencia, wimbo wa Kitambaa Cheupe na mwanamke huyo aliwahi kueleza hilo katika mahojiano yake na Mwananchi Digital, kwamba aliwahi kuonekana katika video ya wimbo huo.
Jambo ambalo limemuibua msanii wa Bongo Fleva, Mr Blue kuzungumzia umuhimu wa ubunifu katika kupeleka ujumbe kwa mashabiki wao, namna unavyowapa thamani kubwa katika jamii.
“Ndiyo maana sikurupuki kuingia studio, natumia akili kuwaza ni kitu gani nikipeleke kwa jamii ili kiwaguse moja kwa moja na kiweze kuishi nao.”
Hilo limeungwa mkono na mkongwe wa Bongo Fleva, Sir Juma Nature aliyesema: “Ili msanii aache alama za heshima katika jamii lazima ujumbe wake uwe na ubunifu mkubwa, mfano wimbo wangu wa Nini Chanzo unaishi hadi sasa, lakini niliuandika miaka mingi nyuma.”