
Mkutano wa Macron na Abbas unakuja mwezi mmoja baada ya makubaliano yanayoyumba kati ya Hamas na Israel ya kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza, baada ya miaka miwili ya mashambulizi ya Israel huko, yaliyosababisha mauaji ya maelfu ya wapalestina. Abbas aliye na miaka 98 ni kiongozi wa muda mrefu wa mamlaka ya wapalestina, iliyo na udhibiti wa sehemu ndogo katika Ukingo wa Magharibi na inatarajiwa kuchukua udhibiti kamili wa Gaza chini ya mpango wa amani wa Trump.
Viongozi hao wawili watajadili hatua zaidi za kuchukuliwa katika mpango huo, hasa katika maeneo ya usalama, utawala, na ujenzi mpya wa Gaza. Macron pia anatarajiwa kugusia umuhimu wa uwepo wa njia salama ya upitishaji wa misaada ya kiutu Gaza, na mabadiliko katika utawala wa eneo hilo. Taarifa kutoka kasri la Elysee, imesema madabiliko ya utawala ni muhimu kwa demokrasia na uhuru wa Palestina ili kuwepo amani na usalama katika maeneo yote mawili, Israel na Palestina.
Mpango huo wa amani wa Trump uliofikiwa Oktoba 10, umepitia changamozo chungu nzima ikiwemo mashambulizi mapya ya Israel huko Gaza na madai ya mashambulizi ya Hamas dhidi ya wanajeshi wa Israel.
Mkutano wa viongozi hao wawili pia unafanyika baada ya Ufaransa mwezi Septemba, kuitambua Palestina kama dola huru katika mkutano wa hadhara kuu wa Umoja wa Mataifa, hatua ambayo Palestina iliipongeza na kuiita ya kihistoria na kijasiri.
Waasi wa Houthi watangaza kusitisha mashambulizi dhidi ya Israel
Huku hayo yakiarifiwa waasi wa Houthi nchini Yemen wametangaza kusitisha mashambulizi yao katika bahari ya Sham dhidi ya meli zinazofungamanishwa na Israel, katika kipindi hiki cha utekelezwaji wa makubaliano ya usitishaji vita Ukanda wa Gaza.
Waasi hao wamesema wanafuatilia hali kwa karibu sana lakini wakaonya kwamba, iwapo adui ataishambulia Gaza wakimaanisha Israel, basi wataanza mara moja mashambulizi yao dhidi ya Israel. Waasi hao wakihouthi wamekuwa wakishambulia meli zinazopita kwenye bahari ya Sharm, katika kile wamekuwa wakisema ni hatua ya kuonesha mshikamano na Wapalestina.
Shambulizi la Hamas la Oktoba 7 2023 Kusini mwa Israel lilisababisha mauaji ya waisrael 1,221 huku mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyofanywa na Israel dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza yakisababisha mauaji ya watu 69,000 wakiwemo wanawake na watoto huku wengine wengi wakiachwa bila makaazi.