Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis  Volker Türk, ametoa wito wa kufanyika uchunguzi huo kuhusu mauaji na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu uliotekelezwa katika muktadha wa uchaguzi wa tarehe 29 Oktoba nchinihumo, kufuatia ripoti kwamba miili ya watu huenda imepelekwa na vyombo vya usalama katika maeneo yasiyojulikana.

Amesema taarifa zilizokusanywa na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kutoka vyanzo mbalimbali nchini Tanzania zinaonesha kuwa mamia ya waandamanaji na watu wengine wameuawa, huku idadi isiyojulikana ya watu wakijeruhiwa au kukamatwa.

Ofisi hiyo imeshindwa kuthibitisha kwa uhuru idadi kamili ya vifo kutokana na hali tete ya usalama na kuzimwa kwa mtandao kulikofuata baada ya uchaguzi.

Tanzania ikabidhi miili ya waliouawa

Türk amesema “Ripoti za familia zinazotapatapa kutafuta wapendwa wao kila mahali, wakitembelea kituo kimoja cha polisi baada ya kingine na hospitali moja baada ya nyingine, ni za kusikitisha sana”

Ameongeza kuwa “Natoa wito kwa mamlaka za Tanzania kutoa taarifa kuhusu hatima na mahali walipo wote waliopotea, na kukabidhi miili ya waliouawa kwa familia zao ili wapate mazishi yenye heshima.”

Ameendelea kusema kwamba “Pia kuna ripoti za kutia wasiwasi kwamba vikosi vya usalama vimeonekana vikiondoa miili mitaani na hospitalini na kuichukua katika maeneo yasiyojulikana, katika kile kinachoonekana kuwa ni jaribio la kuficha ushahidi”.

Kamishna Mkuu huyo wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amezitaka mamlaka za Tanzania kufanya uchunguzi wa kina, huru na wa wazi kuhusu madai haya mazito ya ukiukaji wa haki za binadamu, na kuwawajibisha wote waliohusika.

Aidha, amerejelea wito wake wa kuachiliwa bila masharti kwa viongozi wote wa upinzani waliokamatwa kabla ya uchaguzi mkuu, wakiwemo kiongozi wa chama cha Chadema, Tundu Lissu, na watu wengine wote waliokamatwa kiholela tangu siku ya uchaguzi.

Idadi ya watu waliokamatwa

Inaripotiwa kuwa zaidi ya watu 150 wamekamatwa tangu kura kupigwa, bila msingi wa kisheria ulio wazi huku baadhi yao, wakiwemo watoto, wameripotiwa kufunguliwa mashitaka ya uhaini.

Türk amesisitiza “Ni muhimu kwamba wote waliokamatwa au kuwekwa kizuizini kwa mashitaka ya jinai wafikishwe haraka mbele ya hakimu, na wapewe fursa ya kupinga uhalali wa kizuizi chao. Wote walioko kizuizini lazima wapatiwe haki kamili za kisheria zinazolindwa chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *