“Dunia haipaswi kuiacha Afrika. Dau ni kubwa mno, na uwezo wake ni mkubwa mno,” amesema Guterres akizungumza na waandishi wa habari jijini New York Marekani baada ya Mkutano wa Tisa wa kila mwaka kati ya Umoja wa Mataifa (UN) na Muungano wa Afrika (AU), akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya AU, Mahamoud Ali Youssouf.

Guterres amesema ushirikiano kati ya mashirika hayo mawili “haujawahi kuwa imara kama sasa, na haujawahi kuwa muhimu zaidi.”

Fedha

Ameeleza kuwa Afrika ina historia ndefu kama binadamu mwenyewe, na ina rasilimali nyingi ambazo zimechangia ukuaji wa uchumi wa mataifa mengi, lakini maendeleo yake yanakwamishwa na mfumo wa kifedha wa kimataifa ambao ni wa zamani na usio wa haki.

“Wakati umefika wa kurekebisha mfumo huu wa kifedha ili uakisi hali halisi ya dunia ya sasa na kuhudumia vyema mahitaji ya nchi zinazoendelea, hususan barani Afrika,” amesema.

Ameongeza kuwa mageuzi hayo yanapaswa kuifanya mifumo ya kifedha kuwa jumuishi zaidi, yenye uwakilishi sawa, haki na ufanisi, kwa kutoa nafasi kubwa kwa nchi zinazoendelea kushiriki katika taasisi za kifedha za kimataifa, kuongeza uwezo wa kukopesha wa benki za maendeleo, na kupunguza mizigo ya madeni kwa kutumia mbinu mpya za kifedha.

Guterres pia amerejelea kuunga mkono mpango wa Muungano wa Afrika wa “Kunyamazisha Bunduki” unaolenga kukomesha migogoro barani humo.

Sudan

Kuhusu Sudan, Katibu Mkuu amesema ana wasiwasi mkubwa kutokana na ripoti za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na mauaji ya halaiki mjini El Fasher, pamoja na kuongezeka kwa mapigano katika maeneo ya Kordofan.

“Mtiririko wa silaha na wapiganaji kutoka nje lazima ukatwe. Misaada ya kibinadamu lazima iweze kuwafikia haraka raia wanaohitaji. Mapigano lazima yakome,” amesema Guterres.

Ameyataka majeshi ya Sudan na Kikosi cha Haraka cha Usaidizi (RSF) kushirikiana na Mjumbe wake Maalum, Ramtane Lamamra, kuchukua hatua za haraka kuelekea makubaliano ya kisiasa.

DRC

Amegusia pia hali ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), akisema miongo ya vita imezalisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu ambapo watu milioni 5.7 wamekimbia makazi na wengine milioni 21 wanahitaji msaada wa dharura.

“Wafadhili lazima waongeze misaada yao kwa Mpango wa Mwitikio wa Kibinadamu ambao haujapewa fedha za kutosha. Pande zote za mapigano ziachane na silaha ili mikataba ya amani itekelezwe bila kuchelewa,” amesema.

Amesisitiza kuwa mamlaka na umoja wa DRC lazima viheshimiwe, na mizizi ya machafuko na ukosefu wa utulivu ichambuliwe na kushughulikiwa ipasavyo.

Baraza la Usalama la UN

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika, Mahamoud Ali Youssouf, amesema AU ina dhamira ya kufanya kazi na wadau wote wa Umoja wa Mataifa ili kufanikisha mageuzi ya Baraza la Usalama la UN yenye uwazi, usawa na haki.

“Mageuzi haya ni muhimu sana na yataimarisha zaidi mfumo wa kimataifa wa ushirikiano,” amesema Youssouf.

Ameeleza kuwa mashirika hayo mawili yanakabiliwa na changamoto za kifedha, hivyo ni muhimu kubadilisha namna ya utekelezaji wa programu zao kulingana na uhalisia wa sasa, huku akiweka mkazo katika kuendelea kuunga mkono operesheni za amani, mapambano dhidi ya ugaidi, na misaada ya kibinadamu.

Kuhusu uamuzi wa Marekani kutohudhuria Mkutano wa Kilele wa G20 utakaofanyika Afrika Kusini, Youssouf amesema ni jambo la kusikitisha, lakini akaongeza kuwa bara la Afrika limeamua kuchukua hatima yake mikononi mwao.

“Tunaongeza kujitegemea na tunajenga uwezo wa ndani wa kugharamia maendeleo yetu. Hadithi na mitazamo kuhusu Afrika sasa inabadilika,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *