
Majaji katika kesi dhidi ya kampuni ya Marekani ya kutengeneza ndege, Boeing, iliyoanza Novemba 3 katika mahakama ya kiraia ya shirikisho huko Chicago, Illinois, siku ya Jumatano, Novemba 12, imeamua kampuni hiyo kulipa fidia ya dola milioni 28.45 kwa mjane wa mwathiriwa wa ajali ya ndege ya Ethiopian Airlines 737 MAX 8 ya 2019.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kesi hii, ambayo imekuwa ikifanyika tangu Novemba 3 mbele ya mahakama ya kiraia ya shirikisho huko Chicago, ilikuwa kesi ya kwanza ya kiraia dhidi ya kampui ya ndege ya Marekani ya Boeing baada ya ajali hii na ile iliyotokea mnamo Oktoba 2018, ya ndege nyingine aina ya 737 MAX 8 ya kampuni ya Indonesia ya Lion Air, ambayo iliua watu 346 kwa jumla.
Baada ya takriban saa mbili za majadiliano, baraza la majaji katika kesi ya Boeing lilimpa fidia Soumya Bhattacharya, mjane wa Shikha Garg, mmoja wa waathiriwa wa ajali ya ndege ya Ethiopian Airlines 737 MAX 8, Jumatano, Novemba 12. Mnamo Machi 10, 2019, ndege ya ET302 iliyokuwa ikdafiri kutoka Addis Ababa kwenda Nairobi ilianguka kusini-mashariki mwa mji mkuu wa Ethiopia dakika sita baada ya kupaa, na kuwaua watu wote 157 waliokuwa ndani, ambao walitoka nchi 35 tofauti.
“Tumeridhika na uamuzi huu. Tulikuja hapa kufanya kesi na baraza la majaji, na hii inakubalika kikamilifu,” Bw. Bhattacharya aliambia shirika la habari la Agence France-Presse (AFP) baada ya uamuzi kutangazwa.
Hii ilikuwa kesi pekee iliyosikilizwa hatimaye na baraza la majaji llililoundwa na wanawake watano na wanaume watatu, kwani kesi ya pili iliyopangwa ilikuwa imeamuliwa nje ya mahakama jioni ya siku ya pili ya kesi. Wakili wa Bw. Bhattacharya, Shanin Specter, alikuwa ameomba fidia kati ya dola milioni 80 na dola milioni 230 wakati wa hoja zake za mwisho Jumatano asubuhi.
Kwa upande wake, Dan Webb, wakili mkuu wa Boeing, alikuwa amependekeza dola milioni 11.95 (euro milioni 10.32). Katika hotuba yake ya ufunguzi, alielezea kwamba kampuni ya kutengeneza ndege “ilikubali kwamba Boeing inapaswa kulipa fidia kubwa,” lakini “hatukubaliani tu kuhusu kiasi hicho.” Wakati wa hoja zake za mwisho, alielezea “majuto” ya Boeing kwa waathiriwa na akamgeukia mjane wa Shikha Garg kuomba msamaha kwa niaba ya kampuni hiyo.
“Tunawapa pole sana wale wote waliopoteza wapendwa” katika ajali hizo mbili, msemaji wa Boeing pia alisema baada ya uamuzi huo. “Ingawa tumesuluhisha madai mengi kupitia suluhu, familia pia zina haki ya kufuatilia madai yao mahakamani ili kupata fidia, na tunaheshimu hilo,” aliongeza.