Madrid, Hispania. Nyota watano wa Real Madrid, wanaripotiwa hawana furaha na maisha chini ya Xabi Alonso jambo linaloanza kutishia kibarua cha meneja huyo.

Wachezaji hao ni kipa Thibaut Courtois, winga Vinicius Jnr na viungo Jude Bellingham, Eduardo Camavinga na Fede Valverde.

Vinicius, Bellingham na Courtois inaripotiwa hawapendezwi na mbinu za Alonso hasa ya kuwalazimisha kucheza mpira kuanzia nyuma.

Mastaa hao wanaamini kwamba Alonso anapaswa kuachana na mbinu hiyo na kutumia ile ya kwenda mbele kwa haraka pindi wanapoupata mpira ambayo iliifanya timu hiyo kuwa tishio chini ya Zinedine Zidane na Carlo Ancelotti.

Vinicius Jnr ameonekana kukasirishwa na meneja wake mara kadhaa msimu huu na mfano ni hivi majuzi ambapo alizozana na Alonso baada ya kutolewa nje wakati timu hiyo ilipomenyana na Barcelona.

Valverde na Camavinga wao inadaiwa hawafurahishwi na kitendo cha meneja huyo kutowapa muda mwingi wa kucheza msimu huu.

Pamoja na wachezaji hao kudaiwa hawapendezwi na Alonso, kiungo huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Hispania ameonekana kuwa na mwanzo mzuri msimu huu.

Chini ya Alonso, Real Madrid imepoteza mechi moja tu msimu huu ambao ulikuwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *