Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa umaarufu, sura imekuwa kama kitu cha tofauti na chenye thamani. Watu maarufu wengi hukabiliwa na shinikizo la kuonekana vizuri kila wakati iwe ni mbele ya mashabiki wao, vyombo vya habari au hata familia zao.

Shinikizo hilo mara nyingine huwasukuma kufanya uamuzi mkubwa wa kubadili miili yao kupitia upasuaji. Wengine hufanikiwa na kujisikia vizuri zaidi, lakini kwa wengi mabadiliko hayo huja na madhara ya kiafya, kisaikolojia na hata kijamii.

Mwananchi limekuchambulia baadhi ya watu maarufu waliobadilisha mwonekano wao na madhara waliyopata.

US 01

1. Michael Jackson

Mfalme wa muziki wa pop duniani aliyekuwa na kipaji cha ajabu, MJ alikuwa mmoja ya watu maarufu ambao walijibadilisha mwonekano wake kwa sababu mbalimbali.

Inaelezwa MJ tangu akiwa mtoto katika kundi la muziki wa familia la Jackson 5, alikumbana na shinikizo kubwa kuhusu muonekano wake.

Watu wengi akiwamo dada yake mkubwa La Toya aliwahi kusema kwenye moja ya mahojiano kuwa baba yake, Joseph Jackson alikuwa akimkosoa mara kwa mara Michael kuhusu pua yake kubwa na ngozi yake yenye chunusi. Maneno hayo yalimuathiri kisaikolojia kwa muda mrefu.

Baada ya kupata umaarufu mkubwa, Michael alianza kufanyiwa upasuaji wa kupunguza pua (rhinoplasty) mwanzoni mwa miaka ya 1980. Hata hivyo, hakuridhika na matokeo ya kwanza hivyo akaendelea kufanya upasuaji.

Kadri muda ulivyopita, pua yake ilianza kuwa nyembamba kupita kiasi na hatimaye kuharibika. Ripoti zilisema sehemu ya pua yake ilianza kuvuja na alipoteza sehemu ya mfupa wa asili, jambo lililomfanya atumie kipande bandia cha pua au plasta kufunika.

Kwenye ripoti mbalimbali zinaeleza MJ alifanya upasuaji zaidi ya mara 100 kurekebisha muonekano wake kuanzia pua, kidevu na kusogeza juu macho yake.

Zaidi ya hayo baadhi ya picha zilizowahi kusambaa mitandaoni zilimuonyesha akiwa kwenye kifaa cha kusogeza umri nyuma yaani badala ya kuelekea uzeeni alijirudisha ujanani.

Hata hivyo, upasuaji wa mara kwa mara na matumizi ya kemikali za ngozi vilimletea matatizo makubwa ya kiafya ikiwa ni pamoja na maumivu makali, utegemezi wa dawa za kutuliza maumivu na msongo wa mawazo. Mwishowe maisha yake yalihusishwa zaidi na mabadiliko ya sura yake kuliko kipaji chake cha muziki.

US 02

2. Jocelyn Wildenstein

Ni mwanamke maarufu kutoka Marekani ambaye alipata umaarufu kutokana na upasuaji wake mwingi wa uso. Alianza kuwa na maisha ya kifahari baada ya kuolewa na tajiri mkubwa, lakini baada ya ndoa yao kuanza kuyumba, aliamua kubadilisha muonekano wake kwa njia ya upasuaji wa mara kwa mara.

Inasemekana kwamba alitaka kuonekana kama paka, kwa sababu mume wake alipenda wanyama hao. Kwa hiyo, alifanya upasuaji wa kunyoosha macho, kuongeza mashavu na kubadilisha mdomo mara kadhaa. Hata hivyo, matokeo hayakuwa kama alivyotarajia uso wake ulianza kuonekana usio wa kawaida, na vyombo vya habari vikamuita ‘The Catwoman’.

Madhara yalikuwa makubwa. Kwanza upasuaji mwingi ulimharibu ngozi na tishu za uso na alitakiwa kufanya matengenezo ya mara kwa mara kuiweka ngozi sawa. Pili alikumbana na changamoto kubwa kutoka kwa jamii watu walimcheka na kumdhihaki. Kisa chake kilisababisha msongo wa mawazo mkubwa, upweke na amewahi kupitia changamoto za kifedha baada ya kutumia pesa nyingi kurekebisha muonekano wake.

US 03

3. Donatella Versace

Mbunifu mashuhuri wa mavazi wa Italia ni mfano mwingine wa mtu maarufu ambaye mabadiliko ya mwonekano yalimletea changamoto.

Baada ya kifo cha kaka yake Gianni Versace, Donatella alirithi kampuni na ikawa inamhitaji kuonekana mwenye mvuto mkubwa. Ili kuendeleza hadhi yake katika ulimwengu wa mitindo, alianza kutumia sindano za botox na fillers kwa uso na midomo.

Kadri muda ulivyopita uso wake ulianza kubadilika. Ngozi yake ilionekana ngumu na midomo yake ilipanuka zaidi ya kawaida. Wataalamu wa urembo walisema kuwa alizidisha matibabu jambo lililosababisha uso wake kuonekana kama maski.

Ingawa Donatella hakupoteza mafanikio yake katika tasnia, alikumbana na ukosoaji mkubwa kutoka kwa vyombo vya habari. Watu walijadili zaidi muonekano wake kuliko biashara ya mavazi. Hilo lilimfanya apate msongo wa mawazo na kukaa mbali na TV kwa muda mrefu.

US 04

4. Lil’ Kim

Rapa maarufu kutoka Marekani alianza kubadilika taratibu miaka ya 2000. Kabla ya hapo alikuwa na ngozi nyeusi na sura ya asili, lakini baadaye alianza kuonekana tofauti ngozi nyepesi, pua nyembamba na taya ndogo.

Wengi walimkosoa wakisema hakuipenda asili yake ya mtu mweusi.

Alikiri kwamba alifanyiwa upasuaji kadhaa, akieleza kwamba alikua akihisi hana mvuto kwa sababu ya matukio ya unyanyasaji wa kihisia katika uhusiano na maneno mabaya aliyowahi kusikia kuhusu muonekano wake.

Madhara aliyoyapata yalikuwa kisaikolojia na kijamii. Wengi walimkosoa kwa kujaribu kuwa mtu mwingine wakisema hakuupenda utambulisho wake wa asili wa Kiafrika.

US 05

5. Pete Burns

Pete Burns alikuwa mwanamuziki wa kundi la Dead or Alive, linalojulikana kwa wimbo maarufu ‘You Spin Me Round’. Alijulikana kwa mtindo wa kipekee na ujasiri wa kujaribu muonekano tofauti. Alianza kufanya upasuaji wa uso katika miaka ya 1980 kwa lengo la kuboresha midomo yake.

Hata hivyo, sindano za kuongeza midomo hazikwenda kama alivyotarajia na zilimletea maambukizi makubwa. Midomo yake ilianza kuvimba na kuharibika. Pete alilazimika kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha zaidi ya mara 300 ili kuondoa makovu na kurejesha uwezo wa kula na kuzungumza vizuri.

Alipata maumivu ya muda mrefu na alikiri kuwa alijutia uamuzi wake wa awali. Maisha yake ya kijamii na kazi ya muziki yalitetereka, kwani umma ulianza kumzungumzia zaidi kwa sura yake badala ya kipaji chake.

US 06

6. Heidi Montag

Nyota wa kipindi cha The Hills nchini Marekani, alipata umaarufu akiwa bado kijana. Wakati huo alikuwa anakabiliwa na hofu ya kutoonekana mrembo ikilinganishwa na watangazaji wenzake wa kipindi hicho.

Mnamo mwaka 2009 akiwa na miaka 23 tu, aliamua kufanyiwa upasuaji mara kumi kwa siku moja ambao ni pamoja na kuongeza matiti, kurekebisha pua, lipsi, kuinua nyusi na upasuaji wa taya.

Aliporejea uso wake ulionekana umebadilika kiasi kwamba mashabiki wengi hawakumtambua. Hata yeye mwenyewe baadaye alikiri kwamba alijuta.

Alisema: “Nilihisi kama sifai na nikaamini kuwa sura mpya itanipa furaha. Lakini baada ya upasuaji nilihisi kama nimepoteza uhalisi wangu.”

Madhara aliyopata yalikuwa maumivu makali ya mwili, matatizo ya kupumua na hatari za kiafya kutokana na taratibu nyingi kwa wakati mmoja. Kisa chake kilitumika kama onyo kwa baadhi ya vijana wanaotaka kubadilika haraka kwa sababu ya mitazamo ya urembo wa mitandao.

Wapo watu maarufu wengi ambao walibadilisha mwonekano wao na imekuwa na athari za kudumu. Wengi wao walianza kwa matumaini ya kujihisi vizuri, kujenga kujiamini au kuendana na vile jamii inataka, lakini kwa asilimia kubwa matokeo yamekuwa kinyume wakijikuta kuambulia maumivu, mashabiki kushindwa kuwatambua na msongo wa mawazo.

Kuna funzo kubwa kwenye hilo uzuri wa mtu haupaswi kupimwa kwa sura pekee, bali kwa afya, amani ya akili na uhalisia wa mtu. Upasuaji wa urembo unaweza kusaidia katika hali fulani, lakini unahitaji kufanywa kwa ushauri sahihi wa kitaalamu na kwa sababu sahihi si kwa shinikizo la watu wengine au ulipitia hali fulani.

Michael Jackson alipoteza sehemu ya pua yake, Jocelyn Wildenstein alipoteza heshima, Heidi Montag alipoteza utambulisho wake wa awali, Pete Burns alipoteza afya, na Lil’ Kim alipoteza amani ya nafsi.

WASIKIE WATAALAMU

Daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha maumbile wa Hospitali ya Aga Khan, Aidan Njau anasema madhara ya kufanya upasuaji yanaonekana zaidi kadri muda unavyokwenda.

“Pale unapofanyiwa operesheni unaweza kupata maambukizi na inaweza kukuharibu kuliko ulivyotarajiwa au unaweza kufanyiwa na isiende kama inavyotakiwa, mwili unapoanza kuchoka sehemu uliyofanyia upasuaji inaweza hata kuvuja damu,” anasema na kuongeza

“Kwa wanaofanyiwa kwa urembo labda kuongeza matiti, shepu inaweza kuja kukuletea madhara makubwa, ukavuja damu au muda mwingine shepu uliyoitaka ikaharibika kadri umri unavyokwenda na ukatamani kurudi kwenye hali yako ya kawaida.”

Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Marekani, Jay Calvert anasema: “Upasuaji wa urembo si upasuaji usio na hatari una hatari zilezile za upasuaji mwingine wowote, ikiwamo maambukizi, makovu au matokeo yasiyoridhisha,”

“Wagonjwa wengi hurudi mara ya pili kwa sababu hawakuridhika na matokeo. Mgonjwa anatakiwa afanye utafiti wake mwenyewe kwa sababu madhara ni makubwa kuliko faida ya muda mfupi.”

Prof. Chrysis Sofianos kutoka Afrika Kusini anasema: “Tumeona ongezeko kubwa la upasuaji ulioharibika (botched surgeries) kutoka kwa watu wasio na usajili au elimu sahihi. Wagonjwa wanabaki na makovu, maumivu na wakati mwingine ulemavu kwenye maisha yao,”

“Mitandao ya kijamii na picha zilizochakatwa zimefanya watu wengi kujihisi hawatoshi wakijaribu kubadilisha miili yao kwa sababu zisizo sahihi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *