London, England. Miaka ya nyuma, timu ya taifa ya Brazil ilikuwa ikisafiri kuelekea Kombe la Dunia ikiwa na matarajio ya wazi: kurejea nyumbani na taji hilo linalotamaniwa zaidi katika soka. Haikuwa ajabu kikosi cha mwaka 2002 kilikuwa na washambuliaji hatari kama Ronaldinho, Rivaldo na Ronaldo wakiwa katika ubora wao wa juu.

Timu ya mwaka 1994 iliyolinyakua taji nchini Marekani ilikuwa na nyota kama Cafu, Romario na safu ya ulinzi iliyokuwa imepata uhai upya huku ikiongozwa na Jorginho wa Bayern Munich.

Na bila kusahau vikosi vya 1958, 1962 na 1970 vilivyoongozwa na kijana aliyekuwa hajulikani sana wakati huo Pele.

Lakini safari hii, kuelekea mashindano yajayo yanayofanyika Marekani, Canada na Mexico, Brazil siyo chaguo kuu la wengi. Wamepita miaka 24 bila kubeba Kombe la Dunia, na kwa sasa wanashika nafasi ya saba kwenye viwango vya FIFA. Timu hii iko kwenye kipindi cha mpito, ikijaribu kusonga mbele bila Neymar Jr ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeraha na hajacheza mechi ya kimataifa kwa zaidi ya miaka miwili.

Hata hivyo, ushindi wao wa juzi wa mabao 2-0 dhidi ya Senegal, walio nafasi ya 18 duniani, kaskazini mwa London umeonyesha wazi kuwa Brazil ingawa si ile ya miaka iliyopita hawapaswi kudharauliwa.

Safu yao ya ushambuliaji inayoundwa na Vinicius Jr, Estevao, Rodrygo na Matheus Cunha inatosha kuwatisha mabeki bora duniani. na juzi, katika Uwanja wa Emirates uliokuwa na shamrashamra kama Maracana, wanne hao walikuwa katika kiwango cha juu kabisa.

Katika mfumo wa 4-2-4, kocha Carlo Ancelotti amewapa uhuru mkubwa washambuliaji wake kufanya maajabu mbele wakati Casemiro na Bruno Guimaraes wakisimamia eneo la kiungo. Vinicius na wenzake wanapokuwa katika ubora wao, ni vigumu mno kuwakabili.

Tishio kwa Senegal lilionekana mapema tu baada ya mchezo kuanzaVinicius alipowapita mabeki wawili kwa kasi upande wa kushoto kabla ya kulazimisha kipa Edouard Mendy kufanya kazi ya ziada. Dakika chache baadaye, Cunha alipiga kichwa kilichogonga mwamba.

Lakini kijana Estevao, ambaye Uwanja wa Stamford Bridge uko umbali wa takribani maili tano tu, ndiye aliyefungua hesabu kwa shuti la mguu wa kushoto dakika ya 20.

Hiki ndicho kilele cha Brazil ya Ancelotti. Gabriel na Marquinhos walitengeneza ukuta mgumu katikati, huku Eder Militao akicheza kwa ustadi wa juu.

Senegal walipata nafasi chache mno katika kipindi cha kwanza kabla Casemiro kuendeleza mwamko wake kwa kufunga bao zuri katika ngazi ya mbali kufuatia mpira wa adhabu.

Alipopoteza nafasi yake Manchester United chini ya Erik ten Hag, Casemiro alikaa mwaka mzima nje ya kikosi cha taifa. Hata hivyo, moja ya maamuzi ya kwanza ya Ancelotti kama kocha wa Brazil lilikuwa kumrejesha. Baada ya mechi, Muitaliano huyo alimwelezea kama mchezaji wake muhimu zaidi.

“Alifanya vizuri sana,” Ancelotti alisema.

“Mchezaji muhimu zaidi katika kuleta uwiano tunapokuwa na mpira. Ni mwerevu sana kiufundi, mwenye ubora mkubwa na kiongozi muhimu kwa timu.”

Guimaraes pia hakuwa wa kubezwa; wawili hawa waliutawala mchezo dhidi ya Senegal isiyo katika hali nzuri, ingawa kasi yao inaweza kufanyiwa kazi zaidi dhidi ya timu zenye nguvu.

Lakini Ancelotti ana hazina ya vipaji. Kwenye benchi kulikaa nyota wa Premier League kama Richarlison, Lucas Paqueta, Andrey Santos na Joao Pedro na bado hakumtumia Fabinho, ambaye anaweza kuimarisha kiungo dhidi ya timu kali kama Ufaransa, Uhispania na Uingereza.

Kipindi cha pili kilikuwa na kasi ndogo zaidi huku Senegal wakijitahidi kupitia Sadio Mane lakini bila mafanikio.

Pedro na Paqueta walipata muda wa kucheza lakini hawakuleta mabadiliko makubwa jambo ambalo halitamsumbua sana Ancelotti baada ya kiwango kizuri cha nusu ya kwanza. Mechi ilimalizika 2-0.

Brazil sasa hawajaruhusu bao katika mechi tano kati ya sita chini ya kocha huyo wa zamani wa Juventus, PSG na AC Milan. Mabao waliyofungwa ni yale tu kwenye kichapo cha ajabu cha 3-2 dhidi ya Japan mwezi uliopita wakiwa wametangulia 2-0.

Wanapocheza kwa muunganiko mzuri kama walivyofanya leo, Brazil wana mchanganyiko bora wa ubunifu na uthabiti. Gabriel, Marquinhos na Casemiro wanatoa uzoefu, huku Estevao, Vinicius na Rodrygo wakitoa kasi na ufundi kwenye mashambulizi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *