Kulikuwa na kura 13 za ndio, hakuna kura za hapana  huku Urusi na China zikijizuilia kupiga kura katikati ya wasiwasi kwamba Urusi ingeweza kulipigia kura ya turufu azimio hilo.

Balozi wa Marekani, Mike Waltz, amewashukuru mabalozi akilisifu kama “azimio la kihistoria na la kujenga” ambalo linaweka mwelekeo mpya kwa Mashariki ya Kati.

Uingereza

Uingereza imesema imepigia kura ya ndio azimio hilo kama hatua muhimu katika kuendeleza mpango wa amani kwa Wapalestina, Waisraeli na ukanda mzima, ikilenga “kufungua ukurasa mpya” baada ya miaka miwili ya mgogoro.

Akikumbusha uungwaji mkono mpana wa kimataifa huko Sharm el-Sheikh kwa mpango wa vipengele 20 wa Rais wa Marekani Donald J. Trump na usuluhishi uliofanywa na Qatar, Uturuki na Misri, amesema azimio hilo linausongesha mpango huo mbele, likizingatia pia uungwaji mkono kutoka nchi za Kiarabu na Kiislamu pamoja na Mamlaka ya Palestina.

Amemshukuru Rais Trump na Marekani kwa uongozi wao na kusisitiza hitaji la dharura la kupeleka Kikosi cha Kimataifa cha Kuweka Utulivu, kufungua vizuizi vyote, kuruhusu misaada isiyo na kikwazo, kusaidia ujenzi upya na kuhakikisha kurejeshwa kwa miili ya mateka waliobaki.

Aljeria

Mwakilishi wa Aljeria amesema kwamba amani ya kweli Mashariki ya Kati haiwezekani bila haki kwa watu wa Palestina, ambao wamengoja kwa miongo kadhaa kupata taifa lao huru.

Akitaja kuwa nchi za Kiarabu na Kiislamu zinaunga mkono rasimu hiyo na kwamba Mamlaka ya Palestina imeipokea vizuri, Aljeria imepiga kura kuunga mkono ili kudumisha usitishwaji mapigano na kuunda mazingira yanayowezesha Wapalestina kutekeleza haki yao ya kujitawala na kuwa na taifa lao. Algeria imesisitiza kuwa misaada ya kibinadamu lazima iingie Gaza bila kuingiliwa na kwamba kamati ya kiteknokrasia ya Wapalestina inapaswa kusimamia Gaza hadi Mamlaka ya Palestina itakaporejea.

Aljeria imekitaja Kikosi cha Kimataifa cha Kuweka Utulivu kilichopendekezwa kuwa hatua muhimu kuelekea kuondoka kikamilifu kwa Israel na ikatoa wito wa ujenzi upya wa dharura.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *