Rais huyo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa yupo Brazil kushiriki Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP30.
Kando ya Mto Guamá, kwenye kisiwa cha Combu, msitu mnene umekuwa ukishirikiana kwa karne nyingi na wakazi wa eneo hilo kutoa matunda matamu ya Amazon kama vile cupuaçu, taperebá, peach palm, araçá na zao la kakao.
Ili maliasili hii tajiri au flora iendelee vizazi vijavyo bila vitisho vya mabadiliko ya tabianchi, wajadilianaji waliokusanyika kwenye Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP30, wanapaswa kuhakikisha ulinzi wa misitu.
Minyororo ya uzalishaji ni kitovu cha jamii
Combu ni umbali wa dakika 30 kwa boti kutoka Belém, mji mwenyeji wa Mkutano wa mwaka huu wa mkutano huo wa Umoja wa Mataifa.
Huko, Chama cha Filha do Combu, kilichoanzishwa na Izete Costa, anayejulikana kama Dona Nena, ni mfano wa suluhu za vitendo, zilizotengenezwa na jamii, ili kuokoa sayari dunia.
Jumapili hii, ilikuwa zamu ya rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kukutana na Dona Nena kwa mara ya pili. Ya kwanza ilikuwa alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani.
Alipofika kwenye eneo hilo, aliambia UN News kwamba anafurahi kuona kuwa mpango huo bado unaendelea vizuri na unaokua, ukizalisha “minyororo ya uzalishaji iliyo kitovu cha jamii na kuhakikisha kwamba faida zinaweza kubaki kwa watu wa asili na wakazi wa eneo hilo.”
Mazingira ya ilha do Combu, Belém, Brazil
Tunafanya kazi na msitu ukiwa umesimama
Dona Nena ameeleza kuwa alianza mradi huu akitafuta kubadilisha maarifa ya jadi kuwa chanzo cha mapato, akihifadhi utamaduni wa familia yake na kuchukua kila kitu ambacho msitu unaweza kutoa.
Alilenga kuzalisha chokoleti kutoka kwa zao la kakao ya Amazon, akiuza kwenye masoko madogo. Kisha alijiunga na kozi za ufundi na kupanua biashara, akiongeza kipengele cha utalii, ili watu waweze kutembelea kiwanda cha chokoleti katikati ya msitu. Kati ya wafanyakazi 20 wa kiwanda hicho, 16 ni wanawake.
Uzalishaji wa kakao na matunda mengine hufanywa kupitia mfumo wa kilimo endelevu, ambapo aina kadhaa za asili hushirikiana ili kupata matokeo bora. Kwa mfano, eneo hilo lina miti ya ndizi, ambayo ipo kuvutia nyuki wa kakao.
“Mara nyingi ninaimarisha msitu kwa kile kinachofanya kazi, kwa sababu hapa hatukati msitu kupanda. Tunafanya kazi na msitu ukiwa umesimama na pale ambapo kuna kuporomoka kwa asili, tunatafuta miti, tunapanda.”
Kukuza suluhu
Kiwanda ambacho chokoleti zinazalishwa, na kuzambazwa kote Brazil, hufanya kazi kwa masaa nane kwa kutumia umeme wa jua. Lakini Bi. Nena anataka kuongeza uwezo huu mara mbili, ili kuhakikisha uthabiti zaidi na kuepuka uharibifu wa mashine kutokana na kuzimika kwa umeme, jambo ambalo wakati mwingine hutokea pale ambapo mti unapoporomoka, tatizo ambalo huchukua siku kadhaa kutatuliwa.
Kwa Annalena Baerbock, mradi huu unaonesha kuwa kuna suluhu zinazounganisha ukuaji wa uchumi, maendeleo endelevu na mapambano dhidi ya janga la tabianchi. Kiongozi huyo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amesema kuwa ni muhimu kuunganisha suluhu hizi ili kutimiza ahadi ya kufanya joto duniani kusalia chini ya nyuzi joto 2°C, ikiwezekana 1.5°C.
Rais wa Baraza Kuu Annalena Baerbock akikutana na mjasiriamali wa Brazili mkulima wa kakao Dona Nena katika kisiwa cha Combu karibu na Belém
Matunda yanakauka, kuharibika na kupungua
Hata hivyo, Combu haiwezi kuepuka matokeo ya janga la tabianchi. Dona Nena anasema kuwa katika kipindi cha hivi karibuni, amepata kakao kidogo. Matunda na miti vinakauka na kuharibika. Aidha, hofu kuhusu upungufu wa maji safi inaongezeka kila siku bila mvua.
Ingawa ni msimu wa mvua katika eneo hilo, imepita zaidi ya siku 15 bila tone la maji kuanguka kwenye kisiwa cha Combu.
Rais wa Baraza Kuu amesikiliza kwa wasiwasi mfanyabiashara huyo akieleza ukosefu wa mvua na athari za uzalishaji zilizotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Baerbock amesema kuwa uharibifu wa misitu ni uharibifu wa dhamana ya kuishi kwa binadamu.
Kwake, COP30 inapaswa kuwa “wakati wa kuonesha dunia, hasa katika nyakati za changamoto za kijiopolitiki, kuwa nchi nyingi, pamoja na watu, makampuni na wadau wa kifedha, wanaungana kupambana na janga la tabianchi na, kwa hiyo, kufanikisha maendeleo endelevu kwa wote.”
Rais wa Baraza Kuu la UN Annalena Baerbock akitembea katika msitu wa amazon
Mafunzo kutoka msituni
Baada ya kuonja matunda ya Amazon na mapishi mbalimbali ya chokoleti yaliyotayarishwa pale, Dona Nena alimpeleka Annalena kwenye njia ya msitu, ambapo miaka miwili iliyopita walikutana na kundi la wanawake wazalishaji.
Wamezungumza kuhusu msisitizo ambao mradi unatoa kwa uwezeshaji wa wanawake wakusanyaji, ambao pia wanaweza kuuza bidhaa zao kupitia chama cha Filha do Combu.
Dona Nena amebainisha kuwa, katika kiwanda, wanawake huweka nguvu ya upendo na utunzaji ambayo inachangia mafanikio ya chokoleti.
Msitu ambao ulikuwa sehemu ya mkutano huu pia umewaletea mafunzo muhimu. Wanawake hao wawili waliona pamoja mti wa taperebá ambao ulikua ukikauka kutokana na kuathiriwa na mmea paraziti.
Dona Nena amesema kuwa baada ya mti kufa, mmea huo pia utakufa, kwa sababu utaacha kupata virutubisho vyake. Annalena alibainisha kuwa hii ilikuwa somo la diplomasia, ambalo linaweza kuhusishwa na utoaji wa gesi zinazoharibu sayari.
Lakini pia wamekusanyika mbele ya mti mkubwa wa Kapok wenye umri wa zaidi ya miaka 280. Mti huu mkubwa na wa heshima umesimama tangu kabla ya mazungumzo yoyote ya tabianchi kuanza na utaendelea kuwepo kwa miaka mingi ijayo, ikiwa mazungumzo ya COP30 yatafanikiwa.