
Askalech Abebe, mama wa watoto sita na mwezeshaji wa mazungumzo ya kijamii, amejipambanua kuwa nguzo ya mabadiliko katika eneo analoishi la mkoa wa Kusini-Magharibi mwa Ethiopia. Kupitia video ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya watoto UNICEF, akieleza kwa sauti yenye uzito wa kumbukumbu za uchungu aliopitia alipokuwa msichana.
Bi. Abebe anasema “Wakati ukeketaji unafanywa, macho hufifia na masikio hushindwa kusikia. Ni sehemu ya mwili wetu inayokatwa na kuondolewa kabisa.”
Video inaonesha mikono yake, anafungua kasha dogo, humo ndani ya kasha ndiko kumehifadhiwa kiwembe, taratiiibu anakitoa , kisha anasema;
“Nilikeketwa kwa kutumia kiwembe kama hiki.”
Askalech anakumbuka jinsi ndugu wa mumewe walivyomshinikiza kukeketwa.
“Wakati huo, ndugu wa mume wangu walinifanya nione kana kwamba kutokeketwa ni kosa kubwa.”
“Niliogopa kwamba nisipofanya chochote, ningeweza kufa.”
Lakini leo hii, Askalech ni mfano wa uthubutu na mabadiliko chanya. Ameamua kusimama kidete kupinga mila hatarishi, na sasa anatoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ukeketaji na ndoa za utotoni.
Sasa video ya UNICEF inamuonesha akiwa eneo jingine anatoa elimu kwa wanawake na wasichana, na anasema;
“Tunapokusanyika, tunajadili mambo mengi, hususan ndoa za utotoni na ukeketaji. Nawapa mafunzo ya kina kuhusu madhara yanayoweza kutokea na kuwasihi wawe waangalifu.”
Elimu anayotoa imeanza kuzaa matunda, hasa kwa vijana wa eneo hilo — akiwemo binti yake mwenye umri wa miaka 14, Yemanesh, ambaye sasa ana ujasiri wa kujilinda dhidi ya mila zenye madhara.
“Kutokana na elimu niliyoipata kutoka nyumbani, shuleni, na kutoka kwa mama yangu ambaye hutuongoza sisi na wenzake, nimepata nguvu ya kujilinda.”
Simulizi ya Askalech inafungua macho ya jamii na kuhimiza wazazi na walezi kulinda maisha na mustakabali wa watoto wao wa kike.