Dar es Salaam. Asubuhi  ya kuamkia Ijumaa Novemba 15, 2025 tasnia ya muziki wa dansi ilipatwa na pigo la kuondokewa na mwanamuziki nguli, Boniface Kikumbi Mwanza Mpango maarufu kama King Kiki.

Tangu mwanamuziki huyo afariki dunia hivi sasa umetimia mwaka mmoja na kuwaacha ndugu, jamaa, marafiki na wadau wa muziki wa dansi kutoiona taswira yake.

Nguli huyo alifariki dunia nyumbani kwake Mtoni Kwa Aziz Ally, Dar es Salaam kwa kilichoelezwa na mtoto wake Joseph Silumbe kuwa ni tatizo la saratani ya ini na alizikwa Novemba 18 katika makaburi ya Kinondoni kuhitimisha safari yake ya miaka 77 duniani.

KIN 01

King Kiki alijizolea umaarufu mkubwa kwenye muziki wa dansi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutunga na kuimba nyimbo zenye hisia zenye ujumbe kwa jamii.

Katika Makala haya, tutakupitisha katika hatua mbalimbali ambazo mwanamuziki huyo alizipitia maisha mwake.

KIN 04

KUINGIA NCHINI

Juni, 1970 King Kiki alipata barua kutoka kwa rafiki yake, Freddie Ndala Kasheba aliyekuwa Tanzania wakati huo, akimtaka ashirikiane naye katika masuala ya muziki.

Mwanamuziki huyo akawataarifu wenzake wa bendi ya Super Gabbie juu ya nia yake ya kumfuata Kasheba wa L’Orchestre Fauvette. Super Gabbie 1972 iliingia nchini na kubadili jina na kuitwa Marquis du Zaire.

Bendi hiyo ikamruhusu King Kiki kuja nchini. Wakati huo mwanamuziki huyo alikuwa akiisikia tu Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla na alikuwa akitamani kufika.

Haja hiyo iliongezeka zaidi kipindi ambacho Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Nyerere alipozuru Zaire (sasa Congo DR), enzi za utawala wa Rais wa kwanza wa nchi hiyo, Mobutu Sese Seko Nkuku Ngbendu wa Za Banga. Kiki alimpenda sana Mwalimu ikawa ni fursa. Akiambatana na watu waliomleta Tanzania walipanda meli na kuvuka Ziwa Tanganyika.

Alipofika Kigoma, mshangao wake wa kwanza ulikuwa ni juu ya utamaduni wa Tanzania, alishangazwaa sana alipoliona ni vazi la baibui. Aliwaona kina mama wakiwa wamejitanda mavazi myeusi.

Kisha wakasafiri kwa treni hadi Dar es Salaam. Kina Kasheba walimpokea kwa furaha sana.

Wakiwa Dar, wanamuziki wote wa Fauvette walikuwa wakikaa White House, Ubungo. Bendi hiyo iliyokuwa na wanamuziki hodari kama Kiki, Kasheba, Johnson, Kabala Jojo, Mubaya na wengine, walikubalika na kuzikonga sana nyoyo za mashabiki.

Baadhi ya mashabiki wao walikuwa watu mashuhuri kama vile kina Mzee Kessy Mjinga, Wilfred Mwabulambo, Bhoke Munanka na wengine wengi.

Mwaka 1971, Bendi ya Atomic Jazz ya Tanga iliialika Fauvette ikatumbuize mkoani humo. Atomic ndio iliyoifungulia njia bendi hiyo ya kwenda Kenya kurekodi nyimbo zilizokuja kutamba kama Jacqueline, Zula, Voyage Emonani, Vivi, Maria na Kampala na nyingine. Kisha Fauvette ilirejea na kuendelea kupiga dansi Tanzania.

Mwishoni mwa 1972, bendi hiyo iliondoka Dar es Salaam kwenda Magharibi mwa Tanzania. Mwaka huohuo bendi hiyo ilibadili jina na kujiita Orchestre Safari Nkoy.

Mwaka 1973, Safari Nkoy iliingia Burundi katika Jiji la Bujumbura kisha ikaingia Bukavu mkoani Kivu (Zaire,Congo), ikaenda hadi Goma na Luchuru na baadaye Kinshasa.

Baadaye ikaingia Uganda ikianzia na Kasese, karibu na Ziwa Edward, kisha Mbarara, Masaka hadi Kampala hadi Jinja.

KIN 05

KUBADILI JINA

King Kiki aliachana na Safari Nkoy 1973 na kurudi Zaire kwa lengo la kubadili jina kutokana na amri iliyotolewa na Rais Mobutu.

Mobutu aliwataka raia wa nchi hiyo kurudi Zaire na kuchukua majina ya asili na kuachana na majina ya Kizungu.

KURUDI TENA TANZANIA

Baada ya kutimiza takwa hilo na kubadili jina lake kutoka Boniface na kuitwa jina la Kikumbi Mwanza Mpango ambalo lilikuwa la mjomba wake, alibaki katika miji ya Kinshasa na Kalemie akifanya shughuli za muziki.

Mwaka 1972 Bendi ya Super Gabbie iliingia Tanzania ikitokea Uganda na kubadili jina na kuitwa, Orchester Marquis du Zaire.

Bendi hiyo ilifanya kazi bila Kiki takribani miaka mitano na ilipohitaji kuongezea nguvu ikamtuma, Paul Tshibangu Katai, akamchukue Kiki. 

Ikumbukwe Kiki bado alikuwa na hisa katika bendi hiyo ya Marquis, hivyo aliukubali wito huo na aliongozana na kina Banza Mchafu, Mutombo Sozy, Kanku Kelly Kashama na Ngalula Tshandanda kuja Tanzania.

Akiwa na Marquis du Zaire, Kiki alifanya kazi kubwa na kuanzisha mtindo mpya wa Kamanyola bila jasho. Nyimbo zilizotamba akiwa na Marquis ni kama vile Dora Mtoto wa Dodoma, Nimepigwa Ngwala, Krismas – Bonne Annee, Kasongo, Yoka Mateya ya Baboti, Mokili, Safari Yetu Mbeya na Kyembe. Nyingine ni Saza, Mpenzi Wangu, Kibwe Mutondo na nyinginezo.

Chini ya uongozi wake, bendi hiyo ilipata umaarufu mkubwa na kuongeza mashabiki wengi.

KIN 06

KUJIUNGA NA OSS

Kiki akiwa katika kiwango cha juu kabisa na Marquis du Zaire, mfanyabiashara Hugo Kisima aliihitaji huduma ya mwanamuziki huyo.

Wakati huo, Hugo Kisima alikuwa akimiliki bendi ya Ochestra Safari Sound (OSS) iliyokuwa chini ya mwanamuziki Mbombo wa Mbomboka aliyemtoa Ochestra Makassy. Ikitamba na mtindo wa Nyekese Paralysee 504.

Baada ya mazungumzo yaliyochukua muda mrefu kutokana na kushindana dau, hatimaye Julai 25, 1979, King Kiki aliondoka Marquis du Zaire na kujiunga na OSS kutokana na ushawishi mkubwa wa pesa huku mtangazaji wa Redio Tanzania, Enock Ngombale akitumika kumshawishi.

Inadaiwa kitita cha shilingi 50,000 ndicho kilichomtoa Marguis du Zaire.

KIN 07

MARQUIS WAMSUSIA

Kitendo cha Kiki kutoka Marquis du Zaire hakikupokelewa vizuri na wenzake. Inadaiwa uongozi wa bendi hiyo ulikataa hata nusu ya pesa ya uhamisho ambayo Kiki ilipwe bendi yake hiyo.

Lilikuwa pigo kubwa kwa Marquis kwani hakuondoka peke yake, bali aliambatana na Jean Jacques wengi wanamjua kwa jina la Kabeya Badu, Kanku Nkashama Tubajike ‘Kelly’ na Tshandanda Ngalula. Hata hivyo, Kabeya Badu na Kanku Kelly walirudi Marquis kabla ya kurejea OSS baadaye.

MASANTULA YAZALIWA

Hata hivyo, mara alipoondoka Kasheba ilitoa mwanya kwa King Kiki kutua OSS na kuanzisha mtindo ‘uliosumbua’ sana wa Masantula Ngoma ya Mpwita. Kabla ya kufanya kitu chochote, Kiki alisimamisha maonesho yote ya bendi na kuiingiza kambini.

Mara baada ya mazoezi ya kutosha, OSS ikiibuka na nyimbo zilizopata umaarufu mkubwa sana zikiwemo Mwaka wa Watoto, Mimi ni Safari Sound, Mama Kabibi, Mimi Msafiri, Haruna Kaka, Ni kweli, Krismas Noelle, Mama Kabibi na nyinginezo.

Katika uzinduzi wa albamu hiyo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Safari Resort uliopo Kimara jijini Dar es Salaam kufika saa 12 jioni ulishajaa. Teksi zilikuwa zikipishana na hadi kufika saa 3 usiku hakukuwa na sehemu ya kukanyaga, ilibidi kikosi maalumu cha Jeshi la Polisi kulinda usalama.

King Kiki aliingia ukumbini saa 6 usiku akiwa amevalia joho jekundu na mkononi alikuwa amekamata usinga akiambatana na wanenguaji wawili, Frida Mushi na Ngalula Tshandanda kila mmoja akiwa upande wake.

Ni katika kipindi hicho ndipo mashabiki walimpompachika jina la mfalme ‘King’ na alibaki nalo maisha yake yote ya mbele.

Hali ilikuwa ni tofauti katika Ukumbi wa White House ambapo Marquis ilikuwa ikitumbuiza.

KIN 08

ZENGWE LAANZA

Lakini kabla hata nyimbo za OSS hazijarekodiwa, zengwe lilianza ndani ya bendi hiyo.

Awali Kiki alimkaribisha rafiki yake, Kasheba katika bendi ambaye naye hakuufurahia utawala wa swahiba wake, hivyo maneno ya chinichini yakaanza kutawala ndani ya bendi.

Mipango ya kuung’oa utawala Kiki ulisukwa na Kasheba kwa kushirikiana na wanamuziki wengine bila nguli huyo kufahamu.

Inadaiwa, wanamuziki wengine walikuwa wakidai Kiki alikuwa akijipendelea kwa kuimba na kutunga nyimbo peke yake.

Wanamuziki hao walidai walikuwa na uwezo mkubwa wa kuimba na walishafanya hivyo nyuma ya mwanamuziki nguli wa Congo DR, Mbilia Bell alipokuwa Afrisa International.

Pia, mpambe wa karibu wa bosi Hugo Kisima aitwaye, John Fedha alisema kitendo cha Kiki kuimbisha nyimbo nyingi peke yake kingeweza kuifanya bendi isiwe na mwelekeo mzuri.

“Ikitokea anaumwa hatutaweza kupiga muziki itakuwa hasara,” inadaiwa Fedha aliwahi kutamka maneno hayo.

Katika kitendo kisichotarajiwa ghafla Kasheba akaaaga na kuondoka katika bendi hiyo na kwenda Burundi ambako alikuwa akipiga muziki katika hoteli.

MWISHO WA ENZI, OSS

Mwaka 1981 mkataba wa Kiki na OSS uliisha na hapo akaanza kutengwa na uongozi wa bendi hiyo kwa kutoshirikishwa tena katika masuala ya bendi.

Asubuhi moja, Kiki alipoamka alikutana na kichwa cha habari katika Gazeti la Uhuru kikisema ‘Kiki avuliwa uongozi OSS’. Mwanamuziki huyo alipomfuata Hugo Kisima akajibiwa kutokana na gazeti hilo lilivyoandika, akatakiwa kuwa mwanamuziki wa kawaida, jambo lililomchanganya.

Siku ya pili, Kiki alikutana na kichwa cha habari kingine katika gazeti hilo ambacho kilihitimisha ajira yake OSS.

Kilikuwa ni kichwa cha habari kilichomuumiza sana ’ Kasheba kiongozi mpya OSS’.

KIN 03

AREJEA MARQUIS

Mwaka 1982 King Kiki aliamua kurudi Maquis du Zaire ingawaje haikuwa kazi rahisi kupokelewa.

Mwanamuziki huyo alipewa masharti ya kutunga idadi kubwa ya nyimbo (inadaiwa 1,000) na vilevile hakutakiwa kuwa mwimbaji kiongozi.

Mmoja kati ya wimbo alioutunga ni ‘Nitaendelea’ uliodaiwa kuwa kijembe kwa Kasheba.

Wakati Kiki alipokuwa akinyimwa ushirikiano na uongozi wa OSS, Hugo Kisima alimtuma John Fedha kwenda Burundi kumfuata Kasheba.

UFADHILI MKUBWA

Kiki akiwa Marquis du Zaire alikuwa kama mtu asiyeaminika, alihisi kama vile alikuwa akitengwa na wenzake kutokana na kitendo cha usaliti pale alipohamia OSS, hivyo akaamua kujiweka pembeni.

Inadaiwa rafiki yake, Dk Alex Khalid alikuwa akimfadhili kwa kiasi kikubwa.

Dk Khalid ambaye alikuwa Balozi wa Seychelles (Shelisheli) hapa nchini alimpatia pesa na Kiki kufunga safari ya nchi za Ufaransa na Ubelgiji kwenda kununua vyombo na mwaka 1983 akaanzisha bendi binafsi ya King Kiki Double O iliyokuwa ikitumia mtindo wa Embarasasa Shika- Break.

Bendi hiyo ilipofikia ukingoni, King alipumzika kidogo kisha akafanya kazi na rafiki yake, Kasheba katika bendi ya Zaita Musica, baadaye akajiunga na Sambulumaa akamalizia na ‘ La Capitale Wazee Sugu’ wa Kitambaa Cheupe.

Kiki alizaliwa mwaka 1947, kifo chake kimetokea akiwa na umri wa miaka 77 (sababu ikiwa ni saratani ya ini), kimesababisha huzuni nyingi kwa wapenzi na wadau wa ‘ muziki wa dansi’ wa kada zote.

Kwa zaidi ya miaka 50, King Kiki ametoa burudani kwa Watanzania na amekuwa mlezi na mwalimu wa wengi katika tasnia ya muziki.

Tutamkumbuka na kumuenzi kwa kazi zake nyingi na nzuri ikiwemo wimbo wake maarufu wa ‘Kitambaa Cheupe’ ambao umeendelea kuwa sehemu ya burudani kwenye maeneo na shughuli mbalimbali za burudani nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *