Dar es Salaam. Wilison Nangu ni miongoni mwa wachezaji ambaye hakusajiliwa kwa kelele nyingi kujiunga na Simba, usajili wake ulikuwa ni wa kawaida kutokana na timu aliyokuwa akitokea kuwa ya daraja la kawaida huku na yeye pia akionekana mchezaji wa kawaida, hivyo mashabiki wengi wa Msimbazi hawakuuzingatia sana usajili wa beki huyu aliyetokea JKT Tanzania baada ya kuonyesha kiwango bora na Maafande hao msimu uliopita wa 2024/2025.

Alipotua kwa Wekundu wa Msimbazi kama ilivyotegemewa na wengi kwamba beki huyo asingeweza kupata nafasi ya kutosha kutokana na uwepo wa wachezaji wazoefu kikosini anaochezanao nafasi moja, hivyo akuwa chaguo la kwanza kwa kocha baada kutocheza michezo kadhaa ya mwanzo huku katika nafasi hiyo ya beki wa kati ikionekana kutawaliwa vizuri na Rushine De Reuck, Chamou Karaboue pamoja na Abdulrazack Hamza ambao ndiyo walipewa nafasi zaidi kutokana na uzoefu wao kwenye timu.

Nangu alipata nafasi ya kwanza kuichezea Simba katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate ambapo aliingia kutokea benchi wakati huo Simba ilikuwa chini ya kocha, Fadlu Davids ambaye baadae alitimkia Raja Casablanca. Hata hivyo, bado beki huyo alipata nafasi nyingine tena katika mechi ya hatua ya awali raundi ya kwanza ya kufuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana ambapo Simba iliibuka na ushindi wa bao 0-1 ugenini kabla ya kutoa sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam wakati ikiwa chini ya kocha wa muda, Hemed Morocco ambaye aliisaidia timu hiyo kusonga katika raundi ya pili ya hatua hiyo ya awali.

ALIVYOBADILI UPEPO

Katika mchezo wa raundi ya pili ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika upepo ulianza kumbadilikia Nangu ndani ya Klabu ya Simba ikiwa ni baada ya kupewa nafasi ya kuanza katika mchezo huo muhimu uliopigwa kwenye Uwanja wa Somhlolo dhidi ya wenyeji Nsingizini Hotspurs ambao ndiyo Mabingwa wa Eswatin, Nangu alimuweka benchi Chamou ambaye alionekana kupewa nafasi katika mechi za awali baada ya beki mwenzake Abdulrazack Hamza kupata majeraha.

Kwenye mchezo huo Nangu alifanikiwa kuonyesha kiwango kizuri kutokana na jinsi alivyokuwa akikaba na kushambulia pale timu ilipokuwa ikienda kwenye nusu ya pili ya mpinzani. Hilo alilithibitisha mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kupachika bao la kwanza kwa kichwa na kuipeleka Simba mapumziko ikiwa kifuambele kwa bao moja kabla ya Kibu Denis kuingia kipindi cha pili kuhitimisha karamu ya mabao 3-0 baada ya kufunga mawili.

Katika mechi hiyo ambayo Simba iliibuka na ushindi wa 3-0 ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa Meneja, Dimitar Pantev kusimama kwenye benchi la Msimbazi, pia ikumbukwe kwamba Pantev alitokea Gaborone United ambayo iliondolewa na Simba katika raundi ya kwanza hivyo basi pengine alishawishika kumpa nafasi Nangu huwenda aliuona uwezo wake kwenye mechi hiyo na hata alipotua Simba pengine alithibitisha uwezo wa beki huyo katika viwanja vya mazoezi.

Beki huyo wa kati ambaye pia anauwezo wa kucheza nafasi ya beki wa kushoto aliendelea kuthibitisha makali yake si tu kwa kukaba hata pia kwa kupachika mabao pale anapopata nafasi kwani aliisaidia Simba kupata bao la kusawazisha dhidi ya waajiri wake wa zamani JKT Tanzania, mechi ambayo ilimalizika kwa Simba kushinda 1-2 huku yeye akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo uliopigwa wikendi iliyopita kwenye dimba la Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.

Baada ya mchezo huo kumalzika Nangu alisema licha ya kuanza kupewa heshima na wengi wanaoiona kazi yake uwanjani, lakini haimfanyi abweteke badala yake anaona ana safari ndefu ya kupambana ili huduma yake iendelee kuifaa klabu hiyo.

WAKONGWE WAMBARIKI

Beki wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Amir Maftah alisema kuna kitu anakitengeneza meneja mkuu wa klabu hiyo, Dimitar Pantev akisaidiana na Selemani Matola akibainisha pacha ya Nangu na Rushine De Reuck itakuja kuwa tishio kwa timu pinzani kadri muda unavyokwenda.

“Niliwahi kusema mapema Nangu ni tunu ya Simba kwa baadaye, bado anahitaji muda zaidi, anapewa nafasi anaonyesha kiwango kizuri, jambo la msingi anapaswa kujua kitu ambacho makocha wanakitaka kwake, mfano hiyo pacha wanayojaribu kuitengeneza baina yake na Rushine, maana ni kama Matola na Pantev wanaonyesha wanaiandaa timu ya kushambulia pembeni na kati,” amesema.

Kiungo wa zamani wa Yanga, Pato Ngonyani na sasa anamiliki kituo cha soka cha kukuza vipaji vya vijana kinachojulikana kama Hanga Sports Academy, amesema: “Nangu ni beki mzuri na siyo tu ataisaidia Simba, bali pia timu ya taifa, kikubwa aendelee kupambana na kukilinda kiwango chake na azingatie lengo la kocha kwake ni kitu gani.”

MSIKIE MWENYEWE

Nangu alisema bado ana safari ndefu ya kuendelea kupambana na kila nafasi anayopewa na makocha anatamani iache alama ya kuaminiwa zaidi katika mechi zilizopo mbele yao.

“Kila ninapopata nafasi ya kuwepo uwanjani, kwangu ina tafsiri kitu kikubwa cha kuhakikisha nafanya kazi ambayo makocha watazidi kuniamini na kunipa muda zaidi wa kucheza, Simba ina wachezaji wazuri na wenye ushindani wa juu, unaonisaidia nijitume kwa bidii,” alisena Nangu na kuongeza;

“Kuhusu kuifunga timu niliyokuwa naichezea kabla ya kuja Simba, wakati najiandaa na mechi nilitambua JKT Tanzania ina wachezaji wazuri ila nahitaji kupambania nilipoajiriwa kitu kilichonisaidia kutokuwa na presha.”

Msimu wa 2024-2025 akiwa JKT Tanzania, Nangu alifunga mabao mawili na kutoa pasi mbili za mabao, huku 2025-2026 ndani ya Simba amefunga bao moja la CAF dhidi ya Nsingizini katika mechi ambayo Msimbazi iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 ugenini wakati bao la Ligi Kuu aliifunga JKT Tanzania.

Kwa sasa Nangu yupo katika kambi na kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ambacho kilisafiri kuelekea nchini Misri kujiandaa na mechi ya kirafiki ya kalenda ya FIFA ambayo ilipigwa jana Novemba 15, 2025 dhidi ya Kuwait.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *