Ushindi wa idadi kubwa ya mabao katika mechi za jana usiku, umezihakikishia Ureno na Norway tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitkazofanyika huko Marekani, Mexico na Canada.

Matokeo ya jana yamezifanya timu hizo kuongoza msimamo wa makundi yao na hivyo kuungana na England, Croatia na Ufaransa ambazo tayari zimeshajihakikishia kucheza Kombe la Dunia mwakani.

Katika Uwanja wa Dragao jijini Porto, wenyeji Ureno wameibuka na ushindi mnono wa mabao 91 dhidi ya Armenia ulioifanya ifuzu Kombe la Dunia kwa kuongoza kundi F.

Mbele ya mashabiki 46,702 waliojitokeza uwanjani hapo, Ureno ilifunga mabao hayo kupitia kwa Bruno Fernandes aliyepachika matatu (hat trick) kama ilivyokuwa kwa Joao Neves na mengine yaliwekwa kimiani na Renato Veiga, Goncalo Ramos na Fransisco Conceicao huku bao pekee la Armenia likipachikwa na Eduard Spertsyan.

Kwenye Uwanja wa San Siro jijini Milan, wenyeji Italia walijikuta kwenye mshtuko mkubwa baada ya kukutana na kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Norway.

Kichapo hicho kimeifanya Italia isubirie mechi za mchujo kuwania kufuzu Kombe la Dunia kupitia bara la Ulaya huku Norway ikifuzu kupitia kwenye kundi lao I.

Walioitekeza Italia nyumbani jana walikuwa ni Erling Haaland ambaye alipachika mabao mawili huku mengine yakifungwa na Antonin Nusa na Jorgen Larsen.

Ujerumani, Uholanzi zishindwe zenyewe

Mashindano hayo ya kufuzu Kombe la Dunia kupitia Bara la Ulaya, yataendelea tena leo kwa uwepo wa mechi sita za makundi matatu ya mashindano hayo. Katika kundi A, Ujerumani leo itakuwa nyumbani kuikaribisha Slovakia na Ireland Kaskazini itaikaribisha Luxembourg.

Ushindi wa Ujerumani leo utaifanya ifuzu Kombe la Dunia lakini kama ikifungwa, Slovakia itajihakikishia tiketi hiyo

Kwenye Kundi G, vinara Uholanzi wenye pointi 17 leo watakuwa nyumbani kuikaribisha Lithuania huku Poland inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 14, itakuwa ugenini dhidi ya Malta.

Uholanzi inahitaji ushindi au sare tu katika mechi ya leo ili nayo ijihakikishie tiketi ya Kombe la Dunia. Mechi nyingine za leo ni Montenegro dhidi ya Croatia na Jamhuri ya Czech itaikaribisha Gibraltar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *