Ifakara. Watumishi mpya waliopata ajira siku za hivi karibuni wametakiwa kuwa wazalendo, waadilifu na kuwajibika katika utumishi wao wa umma huku wakionywa kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji Ifakara, Pilly Kitwana wakati akifungua mafunzo ya watumishi wa ajira mpya walioripoti katika halmashauri hiyo kuanzia Februari hadi Oktoba 2025.

“Niwapongeze kwa kupata ajira, mkawajibike katika maeneo yenu ya kazi, mkafanye kazi kwa bidii, mkazingatie maadili ya utumishi wa umma na mkawe wazalendo,” amesema Kitwana.

Aidha mada mbalimbali zilifundishwa katika mafunzo hayo ikiwemo sheria na  kanuni za utumishi wa umma 2022, mfumo wa kujifunza kielektroniki (Muki), muundo wa serikali za mitaa, na masuala ya utawala bora na uwajibikaji.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Coletha Pamba ambaye ni Mhasibu Halmashauri ya mji Ifakara amesema mafunzo hayo yatawasaidia katika utendaji wao wa kazi kwa ufanisi na kuahidi kwenda kutekeleza yale yote watakayoelekezwa na wakufunzi.

Pamba ambaye ni mwajiriwa mpya ameahidi kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu mkubwa na  yuko tayari kufanya kazi katika mazingira yoyote nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *