
Majadiliano kuhusu uhifadhi wa misitu imekuwa moja kati ya ajenda kuu za mkutano wa tabianchi wa COP30.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Misitu ya mvua ya Amazonia na Congo, imekuwa na umuhimu mkubwa katika kuisaidia dunia kukabili mabadiliko ya tabianchi, kutokana na uwezo wa kufyonza hewa ukaa kutoka kwenye anga, pamoja na utajiri wa bayoanuai ambayo ni muhimu katika mazingira.
Shirika la Greenpeace limekuwa likifuatilia hali ya ukataji miti kwenye msitu wa mvua wa Congo.
Bonaventure Bondo ni miongoni mwa wanaharakati wanaoendeleza kampeni kuhusu kuulinda msitu huo, anasema kuna haja ya nchi zinazopatikana katika eneo la Congo Basin kuzungumza kwa sauti moja katika mkutano wa COP30.
“Ni muhimu kwa nchi za Congo Basin kuhakikisha msitu wa mvua wa Congo unasalia katika hali nzuri, sio tu kwa sababu ya kukabili mabadiliko ya hali ya hewa lakini pia kwa sababu ya haki za jamii za kiasili zinazotegemea msitu huo. Nchi za Congo Basin zinatakiwa kuungana na kuzungumza kwa sauti moja.” Alisema Bonaventure Bondo mwanaharakati wa mazingira.
Aidha Bondo anasema haki za jamii za kiasili katika msitu wa mvua wa Congo zinapaswa kulindwa.
“Tunasheria nchini DRC inayowalinda watu wa jamii za kiasili wanaoishi kwenye misitu, kinachokosekana ni utekelezwaji.Tunatoa wito kwa serikali ya DRC kuhakikisha sheria hiyo inaheshimiwa ili kuzifanya jamii hizo kuhisi zinalindwa kwenye ardhi yao.’’ Alisisitiza Bondo.
Mashirika ya kulinda mazingira nchini DRC yamekuwa yakepinga mradi wa serikali ya Kinshasa wa kuchimba mafuta, mashirika hayo yakihofia athari za mradi huo kwa mazingira.
Kamate Francoise mwanaharakati kutoka shirika la Congo Basin Alliance.
“Muda umefika wakukataa kabisa uchimbaji wa mafuta katika msitu wa Congo kama njia moja ya kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.” Alisema Kamate Francoise.
Kuhusu suala la uhifadhi wa misitu mashirika tofauti ya mazingira sasa yanasema kuwa ufadhili kwa ajili ya kulinda misitu ni lazima uambatane na sera madhubuti.
Minzilet Ijai, Belem, RFI Kiswahili.