
Kutofanikiwa kwa baadhi ya timu kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 huko Marekani, Canada na Mexico, kutafanya nyota baadhi wa soka kutoonekana katika mashindano hayo ambayo ni ndoto ya kila mchezaji duniani kushiriki.
Wachezaji hao watalazimika kuwatazama wenzao kwenye luninga wakiwa na jezi za timu zao za taifa hapo mwakani na baadhi watalazimika kusubiri hadi Fainali za mwaka 2030 kuona kama wanaweza kutimiza ndoto hiyo.
Katika idadi kubwa ya wachezaji ambao hawatokuwepo kwenye Kombe la Dunia mwakani, Mwananchi Digital inakuletea orodha ya nyota 10 wanaotamba kwenye soka duniani hivi sasa ambao timu zao zimeshindwa kufuzu Kombe la Dunia.
VICTOR OSIMHEN (Nigeria/Galatasaray)
Mabao nane ambayo ameifungia Nigeria katika mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia, hayajatosha kumfanya nyota huyo aliyeibuka Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Uturuki msimu uliomalizika.
Ni mara ya pili mfululizo kwa Nigeria kutofuzu Fainali hizo ambapo mara ya mwisho ilishiriki za mwaka 2018 huko Russia.
BRYAN MBEUMO (Cameroon/Manchester United)
Nyota wa Cameroon, Bryan Mbeumo amekuwa na kiwango bora kwa sasa akiwa na kikosi cha Manchester United ambapo tayari ameshaifungia timu hiyo mabao matano katika mechi 11 alizoichezea kwenye Ligi Kuu England (EPL).
Hata hivyo Mbeumo hatoonekana katika Kombe la Dunia mwakani kwa vile Cameroon haijafuzu ambapo imeishia hatua ya mchujo.
PIERRE-EMERICK AUBAMEYANG (Gabon/Marseille)
Amefunga mabao sita na kupiga pasi mbili ya mwisho katika mechi 10 za Ligi Kuu ya Ufaransa msimu huu.
Katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia, ameifungia Gabon mabao saba lakini hayajatosha kuifanya ifuzu.
SERHOU GUIRASSY (Guinea/Borussia Dortmund)
Guinea imemaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa kundi G la kuwania kufuzu Kombe la Dunia kwa upande wa Afrika ambalo Algeria ilimaliz ikiwa kinara.
Kwa maana hiyo, mashabiki hawatomshuhudia nyota wa Borussia Dortmund, Serhou Guirassy.
ADEMOLA LOOKMAN (Nigeria/Atalanta)
Msimu uliopita aliingia katika kikosi bora cha Ligi Kuu ya Italia kutokana na kiwango bora alichoonyesha akiwa na Atalanta na kwenye mechi za kufuzu Kombe la Dunia amecheza mechi 12 akipiga pasi mbili za mwisho.
Kama ilivyo kwa Osimhen, kutofuzu kwa Nigeria kwenye Kombe la Dunia 2026 kutamfanya Lookman asicheze mashindano hayo.
BENJAMIN SESKO (Slovenia/Manchester United)
Slovenia ilimaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi B la kufuzu Fainali za Kombe la Dunia kupitia Ulaya hivyo nyota wa manchester United, Benjamin Sesko hatokuwepo kwenye Kombe la Dunia.
CONSTANTINOS TSIMIKAS (Ugiriki/AS Roma)
Kutofuzu kwa Ugiriki kwenye Fainali zijazo za Kombe la Dunia, kutafanya beki wa zamani wa Liverpool, Constantinos Tsimikas kuzitazama fainali hizo kwenye luninga.
DOMINIK SZOBOSZLAI (Hungary/Liverpool)
Dominik Szoboszlai amekuwa na kiwango bora hivi sasa ndani ya jezi ya timu ya Taifa ya Hungary na klabu yake ya Liverpool katika msimu huu.
Hata hivyo Hungary haijafuzu Kombe la Dunia baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye Kundi F la kuwania kufuzu Kombe la Dunia.
DUSAN VLAHOVIC (Serbia/Juventus)
Nyota wa Juventus ya Italia, Dusan Vlahovic hatakuwa miongoni mwa mastaa ambao watakosekana katika Fanali zijazo za Kombe la Dunia kwa vile timu yake ya Taifa ya Serbia, haijafanikiwa kufuzu.
YVES BISSOUMA (Mali/Tottenham Hotspur)
Mali haijafanikiwa kufuzu Fainali zijazo za Kombe la Dunia hivyo kiungo Mkabaji wa Tottenham Hotspur, Yves Bissouma kwa mara nyingine tena anakosa kwenda katika fainali hizo.