
Nchini Nigeria, idadi isiyofahamika ya wanafunzi kutoka Shule inayomimilikiwa na Kanisa Katoliki, wametekwa na watu wenye silaha, katikati ya nchi hiyo, ikiwa ni tukio la pili kufanyika wiki hii.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Utekaji huo umetokea katika Shule ya Mtakatifu Maria,katika eneo la Papiri, jimboni Niger, ambapo maafisa wa usalama walikuwa wameagiza kufungwa kwa shule zote za mabweni kwa sababu za kiusalama.
Mpaka sasa haijafahamika ni wanafunzi wangapi walitekwa, lakini wakaazi wa eneo hilo wanasema, wanafunzi 100 na walimu huenda wamechukuliwa na watu hao wenye silaha.
Ripoti zaidi zinasema, wanafunzi hao walivamiwa saa nane usiku wa kuamkia Ijumaa na kutekwa na watu wasiofahamika, waliokuwa na silaha.
Ni wiki hii tu ambapo utekaji mwingine, ulifanyika katika jimbo jirani la Kebbi, ambapo wanafunzi zaidi ya 20 walitekwa wakiwa Shuleni.
Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, aliahirisha ziara zake nje ya nchi wiki hii, ili kushughulikia matukio ya utekaji katika taifa hilo la Afrika Magharibi lenye wingi wa watu.