Katika taarifa aliyoitoa kupitia ukurasa wake wa X, Bi. Amina J. Mohammed amesema ameshtushwa sana na tukio hilo, akisisitiza kuwa “shule zinapaswa kuwa mahali salama pa elimu, si maeneo ya mashambulizi dhidi ya wasichana.” Ameiitaka serikali kuhakikisha wanafunzi wote waliotekwa wanarejeshwa mara moja, akiongeza kuwa “Ni lazima tulinde shule na kuwawajibisha wahalifu. Ukatili dhidi ya watoto wote haukubaliki.”
Wanafunzi katika shule moja ya msingi mashariki mwa Nigeria wakisubiri mwalimu aingie masomo yaanze.
Idadi ya waliotekwa
Kwa mujibu wa duru za habari Jumuiya ya Wakristo Nigeria CAN imetoa idadi mpya leo Jumamosi, ikiripoti kuwa wanafunzi na walimu 315 walitekwa na watu wasiojulikana. Idadi hii ni kubwa zaidi kuliko makadirio ya awali na inaonesha ukubwa wa tukio hilo, ambalo sasa limekuwa utekaji wa pili wa shule ndani ya wiki moja nchini humo.
Jumatatu wiki hii, washambuliaji waliwateka wasichana 25 kutoka shule ya sekondari katika Jimbo jirani la Kebbi, tukio lililozidisha hofu kuhusu kuongezeka kwa ukosefu wa usalama na mashambulizi yanayolenga taasisi za elimu kaskazini mwa Nigeria.
Hakuna kundi lililodai kuhusika na matukio haya mawili hadi sasa.
Wachambuzi wa masuala ya usalama na wakazi wa eneo hilo wamefananisha utekaji huu wa Jimbo la Niger na ule maarufu wa Chibok mwaka 2014, wakati wasichana karibu 300 walipotekwa na waasi wa Boko Haram katika Jimbo la Borno.
Zaidi ya muongo mmoja baadaye, baadhi ya wasichana hao bado hawajapatikana kumbukumbu chungu ya madhara ya muda mrefu kwa waathiriwa, familia na jamii.
Baada ya miaka miwili ya kushikiliwa na kundi la Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa Nigeria, mmoja wa wasichana wa Chibok akieleza hali mbaya aliyokutana nayo.
Wito wa kuimarisha ulinzi mashuleni
Matukio haya mapya yamefufua wito wa kuimarisha ulinzi katika shule zilizopo maeneo yanayokabiliwa na makundi yenye silaha, ujangili, na ukatili wa misimamo mikali.
Mamlaka zinasema juhudi za uokoaji zinaendelea, lakini taarifa bado ni chache.
Bi. Mohammed ametoa wito kwa serikali ya Nigeria na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua Madhubuti ili kuhakikisha “Wanafunzi waliotekwa nchini Nigeria kwa miaka mingi na sasa, lazima waachiwe mara moja.”
Wakati familia zikiendelea kusubiri taarifa za wapendwa wao, shinikizo linaongezeka kwa serikali kuzuia kurudiwa kwa misururu ya utekaji wa wanafunzi ambayo imelitikisa taifa hilo la Afrika Magharib kwa zaidi ya miaka kumi.